Tanzania yang’ara fainali futsal Ufilipino

UFILIPINO; TIMU ya taifa ya wanawake ya mchezo wa futsal leo Novemba 26, 2025 imepata ushindi wake wa kwanza kwenye michuano ya kombe la dunia kwa kuifunga New Zealand mabao 4-2.

Dalili za ushindi kwa Tanzania zilionekana tangu mwanzoni mwa mchezo huo kwenye Uwanja wa Philsports Arena mjini hapa kwa wachezaji wake kulisakama lango la New Zealand tangu mwanzoni mwa mchezo.

Mabao ya Tanzania  yaliwekwa kimiyani na Mary Siyame aliyefunga mabao matatu na moja likifungwa na Winfrida Mathius. Mary pia alitwaa tuzo kwa kuibuka mchezaji bora wa mechi hiyo.

Matokeo hayo yanaisogeza Tanzania hatua moja mbele kwenye mchezo huo kwani ilipoteza mabao 10-0 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Ureno.

Tanzania sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi C ikiwa na pointi tatu sawa na Japan iliyo nafasi ya pili iliyofungwa mabao 3-1 na Ureno leo, hivyo Ureno kuendelea kuwa kinara wa kundi hilo kwa kufikisha pointi sita.

New Zealand inashika mkia ikiwa haina pointi baada ya kupoteza mechi zote mbili.

Tanzania na Japan zinatarajiwa kukutana Jumamosi katika mechi ya mwisho ya makundi, mechi inayotarajiwa kuwa ya vuta nikuvute kwani timu zote zinahitaji ushindi ili kufuzu robo fainali.

Akizungumzia matokeo ya mechi hiyo Kocha Mkuu wa Tanzania Curtis Reid amesema ana furaha kubwa kuona wachezaji wake wanamuelewa kila anapowafundisha jambo.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button