“Tumeendelea kudhibiti mfumuko wa bei”

IKULU: RAIS Samia Suluhu Hassan amesema baadhi ya mafanikio ambayo Tanzania imeyapata katika mwaka uliopita kuwa ni amani, ulinzi na usalama nchini kwa kuwa mipaka ya nchi ilikuwa salama.

Ameeleza mafanikio hayo katika sehemu ya salamu zake kwa Watanzania katika kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2024.

Advertisement

 

Amegusia pia mapito ya kiuchumi duniani kutokana na UVIKO 19 na athari za vita yalisababisha mfumuko wa bei hususani wa chakula na mafuta ya vyombo vya moto na kuvuruga mnyororo wa ugavi wa kimataifa, kupanda kwa riba kwenye masoko ya fedha na kuathiri upatikanaji wa Dola za Marekani.

“Tumeendele kudhibiti mfumuko wa bei ambao katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2023 ulipungua hadi wastani wa asilimia 3.9 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 4.3 kipindi kama hicho mwaka jana, 2022,” amesema Rais Samia.

Amesema ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa mwaka jana ulikadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 2022.

 

Serikali ilipokea Dola za Marekani bilioni 1.3 sawa na shilingi trilioni tatu mwaka 2022/23 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo sawa na asilimia 100 ya kiasi kilichopangwa kukopwa.

Amesema serikali iliweka mazingira rafiki ya kibiashara na kuwezesha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kusajili miradi 504 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.6 ambayo ni ongezeko la asilimia 58 ikilinganishwa na miradi 292 mwaka juzi.

Kuhusu ukusanyaji wa kodi, Rais Samia amesema kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni mwaka jana, ukusanyaji ulifika Sh trilioni 22.6 sawa na ongezeko la asilimia nane ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka juzi huku bajeti ya kilimo iliongezeka kutoka Sh bilioni 751 mwaka juzi hadi Sh bilioni 970 mwaka jana.

Mafanikio mengine ni kwenye sekta ya utalii ambapo Tanzania ilipokea watalii milioni 1.8 Oktoba mwaka juzi hadi Oktoba mwaka jana ikilinganishwa na watalii milioni 1.4 mwaka juzi na mapato yaliyopatikana ni Dola za Marekani bilioni 3.22 ikilinganishwa na Dola bilioni 2.33 kipindi kama hicho mwaka juzi.

 

Amezitaja sekta nyingine ambako kulikuwa na mafanikio ni afya ikiwemo kuboresha huduma za kibingwa na vifaa tiba, sekta ya maji kwa kukamilisha miradi 506 yenye uwezo wa kuhudumia wananchi milioni 5.8, sekta ya elimu kwa kuendeleza miundombinu ya shule, kuongeza bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu hadi kufikia Sh bilioni 731 kutoka Sh bilioni 654, kutoa ufadhili wa masomo kupitia Samia Scholarship kwa kutenga Sh bilioni 6.7 mwaka jana na kunufaisha wanafunzi 1,019.

 

Amesema kutokana na ushirikiano mzuri na nchi na mashirika ya kimataifa, Tanzania imefanikiwa kupata Dola za Marekani milioni 550 kwa ajili ya miradi ya usalama wa chakula, Dola milioni 297.64 za mradi wa mawasiliano vijijini, Chuo cha Teknolojia cha IIT Madras kutoka India na Dola milioni 500 kutoka Benki ya Dunia kusaidia bajeti ya Serikali.