Samia ataja utumishi wa dini unaofaa
RAIS Samia Suluhu Hassan amelipongeza Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa huduma inazotoa katika jamii, akisema huo ndio utumishi wa dini unaotakiwa.
Rais Samia amesema hayo kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Watoto Wenye Mahitaji Maalumu cha Kitopeni – Bagamoyo Diaconic Lutheran Centre, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Aidha, ameliomba kanisa hilo kuliombea taifa hasa wakati huu linapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
“Nimependa sana mstari uliosoma Baba Askofu (Mkuu wa Kanisa, Dk Alex Malasusa) unaosema, Amin Amin nawaambia, kadri mlivyomtendea mmoja wa hao wadogo mlinitendea mimi,” alisema Rais Samia.
Alisema ujumbe huo ndio umebeba dhima nzima ya harambee hiyo kwamba jamii yote inapaswa kushiriki katika kujali wenye mahitaji maalumu na ya kawaida katika jamii.
Alisema kazi iliyoanzishwa na kanisa hilo imeonesha kutekeleza mafunzo ya maisha na matendo ya miujiza ya Yesu Kristo kwani kanisa halikuishia kuonesha huruma na kuwahudumia wenye mahitaji kiimani,
bali kama alivyofanya Yesu Kristo nalo limewasaidia na kuwaletea mahitaji kwa kuwalisha, kuwavika na kuwatembelea.
“Hili ndilo jukumu letu sote… kuwavika, kuwalisha na kuwatembelea wagonjwa na kuwapa wenye mahitaji. Kanisa limefanya mengi zaidi ya haya, nalipongeza sana na huu ndio utumishi wa dini,”alisema Rais Samia.
Alisema kazi hiyo inayofanywa na KKKT inapeleka ujumbe kwa wengine kuwa utumishi wa dini ndio huo kusaidia na kujenga jamii iliyo bora na si kufanya matendo yasiyofaa.
Alisema katika kazi hiyo iliyoanzishwa na kanisa serikali inaunga mkono na itakuwa bega kwa bega kusimamia na kuendesha kituo hicho ili malengo yake yatimie.
Aliwataka Watanzania kuchangia harambee hiyo ili kufikia lengo lake la kupata kituo cha kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu ambao jamii imekuwa ikiwatenga.
Katika harambee hiyo, Rais Samia alichangia Sh milioni 100 na washauri wake pamoja na yeye binafsi walichangia Sh milioni 150 nyingine.
Awali, Mkuu wa KKKT ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa alisema wamepata ahadi na fedha taslimu zaidi ya Sh bilioni 6.5 zitakazotumika kujenga kituo hicho cha watoto Kitopeni, Bagamoyo mkoani Pwani.
Dk Malasusa alisema ndoto ya kanisa ni kuona kituo hicho kinakamilika na kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalumu wakiwamo wenye ulemavu wa akili, mtindio wa akili na wengine kama hao.
Alibainisha kuwa kitahudumia watoto wote wenye changamoto hizo katika jamii bila kubagua dini, familia au rangi na kuwasihi wananchi kutowaficha watoto hao ndani, bali wawapeleke kwenye vituo vya huduma kuelimishwa na kupata mafunzo yanayowasaidia kujitegemea.
Katika harambee hiyo, wadau mbalimbali walichangia wakiwamo Benki ya CRDB iliyotoa Sh milioni
100, NBC Sh milioni 50, NMB Sh milioni 50, mashirika ya umma Sh milioni 150, Benki ya Maendeleo Sh milioni 140, Profesa Kitila Mkumbo Shmilioni 10, Wizara ya Fedha Sh milioni 10 na wadau wengine.
Katika harambee hiyo, wakuu wa majimbo yote ya kanisa hilo ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani waliwasilisha hundi ya mfano ya Sh bilioni 2.7 zilizotolewa na waumini wao. Gharama za ujenzi wa kituo hicho ni Sh bilioni sita.



