Samia Housing Scheme kuzalisha ajira 26,000
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) wameweka wazi takribani ajira 26,000 zinatarajiwa kuzalishwa katika mradi mpya wa ujenzi wa nyumba unaofahamika kama Samia Housing Scheme unaotekelezwa kwa ghaarama ya Sh bilioni 466.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Mauzo na Masoko Mwandamizi wa NHC, Daniel Kura wakati akizungumuza na waandishi wa habari katika viwanja vya Maonyesho ya Tano ya Teknolojia ya Madini mjini Geita.
Ameeleza mradi huo unatekelezwa kwa awamu nchi nzima ambapo ujenzi wa nyumba utaanzia Dar es Salaam na baadaye kuhamia Dodoma ambapo takribani nyumba 5,000 zinatarajiwa kujengwa kupitia Samia Housing Scheme.
“Kwa hiyo tumekuja kwenye maonyesho haya ili wananchi wawe na taarifa sahihi na tunakutana na taasisi na makampuni mbalimbali tuwape taarifa na wale wote wenye mahitaji ya nyumba waweze kupata huduma kwa wakati.
“Mradi huu utagusa madaraja yote kwa maana ya daraja la chini, daraja la kati na daraja la juu, lakini kwa ujumla ni mradi ambao umeangalia vipato vya watanzania wote wawe ni watumishi katika sekta ya umma, watumishi sekta binafsi ama wawe ni wafanyabishara.”
Mkuu wa Kitengo cha Habari wa NHC, Domina Rwemanyira amesema wanaendelea kutekeleza mradi huku wakilenga kuyafikia makundi yote ya watanzania ingawa gharama ya pango inaongezeka kutokana na gharama za ujenzi.
Domina amefafanua mradi unatekelezwa kwa miezi 24 lakini gharama ya nyumba ama pango itategemea na maeneo miradi inapotekelezwa yanamilikiwa na Halmashauri na yamekuwa nje kidogo ya mji hivo usogezaji wa huduma unaongeza gharama.