Samia Kagera Cup kuchagiza uchaguzi mitaa

MASHINDANO ya mpira wa miguu ya ‘Samia Kagera Cup’ yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi mkoani Kagera yakiubeba ujumbe wa elimu mahususi ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Akizungumza leo Novemba 8, 2024 mwanzilishi wa mashindano hayo, Leonard Kachebonaho ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa UVCCM Taifa amesema mashindano hayo yatahusisha halmashauri nane za Kagera yakihamashisha masuala kadhaa ikiwemo ya uchaguzi wa mitaa.

Advertisement

Amefafanua kuwa kamati husika iliyaita mashindano hayo jina la Rais Samia kutokana na mambo mengi ya kimaendeleo yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika kwa Kagera hivyo  wakaona umuhimu wa mashindano hayo kuyapatia jina hilo la Samia Kagera Cup kama pongezi kwake.

Amezitaja zawadi kwa washindi ambapo mshindi wa kwanza atapokea Sh milioni 10 mshindi wa wapili Sh milioni  5 na mshindi wa watatu Sh milioni 3.

Hata hivyo Kachebonaho amemshukuru  Mkuu Wa Mkoa Kagera kwa jinsi alivyobariki ligi hiyo bila kuwasahau na wadau mbalimbali ambao wamejitokeza kuunga mkono mashindano hayo.

“Mashindano hayo yanalenga kuwavutia vijana kushiriki kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa sisi tunasema tusiishie kijiandikiasha lazima tushiriki pia kupiga kura ili kupata haki zetu kikatiba na kupata viongozi bora ,tunaamini hii ligi  itakuwa na mvutio wa kutosha na kuwaunganisha vijana wengi, “amesema kachebonaho

Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwassa awali amepongeza wazo la mashindano hayo ambapo alisema  wao kama serikali watakuwa na ligi hiyo bega kwa bega ili kuhakikisha inafanikiwa vyema.

Al Amini Abdul ni katibu wa chama cha mpira wa miguu Kagera amesema mashindano hayo yataanza tarehe 9 Novemba na kukamilika Tarehe  23 Novemba mwaka huu 2024 katika viwanja vya Kaitaba Mjini Bukoba.