JUZI Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na kufanya mazungumzo na mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao Tanzania.
Katika mazungumzo hayo Dar es Salaam, Rais Samia alisema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025, Serikali itaendeleza majadiliano ya kisiasa miongoni mwa Watanzania wote.
Kuonesha dhamira yake njema, aliwaambia wanadiplomasia hao kuwa atawajuza kila kitakachokuwa kinaendelkea
wakati wote wa uchaguzi.
Pamoja na faida nyingine, kufanya hivi pia, kutawafanya wawakilishi hao nchini kupata taarifa rasmi na sahihi kuhusu kinachotokea.
Tunampongeza Rais Samia kwa dhamira njema anayoendelea kuonesha na kuhakikisha falsafa yake ya ‘4R’ inaendelea kutumika na kusaidia ujenzi wa taifa kupitia maridhiano, uvumilivu, mageuzi na ujenzi mpya wa taifa.
Sisi tunampongeza kwa kuendeleza dhamira yake kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa 2025 unakuwa huru na haki na kwamba kila mtu au kila chama, kinavuna kilichopanda kwa Watanzania kupitia sanduku la kura maana aliyepanda
matendo atavuna matendo na aliyepanda maneno, atavuna maneno.
Tunampongeza Rais Samia kuendelea kukumbatia falsafa ya 4R maana tangu ianze kutumika alipoingia madarakani, imeonesha matunda bora kwa kuimarisha demokrasia miongoni nchini hali inayochochea ujenzi wa pamoja wa taifa kupitia mshikamano na umoja wa kitaifa.
Tunasema, wanaofuatilia siasa na demokrasia nchini Tanzania na hususani wenye dhamira safi, wanakiri kuwa falsafa ya 4R imeleta mageuzi ya kisiasa na kufanya mchakato wa uchaguzi wa kisiasa nchini kuwa bora zaidi na wenye mvuto kwa Watanzania.
Tunasema, mfano mzuri umedhihirika katika mwitiko na ushiriki wa Watanzania katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 27, mwaka jana.
Kimsingi, juhudi alizoanza na anazoendelea kufanya Rais Samia kupitia falsafa hiyo hususani katika vipengele vya
maridhiano na uvumilivu kuwezesha mageuzi na ujenzi mpya wa Tanzania, ni njia anayosafishia Watanzania kuelekea ushiriki kamilifu wa mchakato wa uchaguzi mkuu ujao.
Kwa kusema hivi tunasema, Watanzania waoneshe moyo wa shukrani kwa kujiandaa kushiriki kikamilifu mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025 kwa amani ili uchaguzi uwe huru, haki na wa amani kama anavyodhamiria mkuu wa nchi.
Kufanikisha hili, Watanzania katika maeneo yao mbalimbali wajitokeze kujiandikisha au kurekebisha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kadiri Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar zinavyofika katika mikoa na maeneo yao kwa kazi hiyo.
Watanzania wajitokeze katika mikutano ya kampeni kusikiliza ‘mchele’ na ‘pumba’ za baadhi ya wanasiasa ili siku
ya siku inapowadia, wapige kura kuchagua viongozi bora kwa busara na si kwa mihemuko.
Ndio maana tunasema, Rais Samia anazidi kusafisha njia ya Watanzania Uchaguzi Mkuu 2025.