RAIS Samia Suluhu Hassan yuko nchini Ethiopia kushiriki Mkutano wa kawaida wa 38 wa Wakuu wa Nchi na serikali wa Umoja wa Afrika (AU).
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga amesema kwenye taarifa yake kuwa pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili ajenda kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyopendekezwa na Tanzania.
Rais Samia ni kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi Afrika na kwa mwaka jana alizindua kampeni ya miaka 10 nchini kuhakikisha ifikapo 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Kabla ya kushiriki mkutano wa 38, Rais Samia atashiriki mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika utakaofanyika Februari 14, 2025,” amesema Sharifa kwenye taarifa yake.
Taarifa hiyo ya Ikulu ilisema mkutano huo wa AU unaofanyika kuanzia Februari 14 hadi 16, pia unatarajiwa kuchagua mwenyekiti mpya atakayechukua nafasi ya Mohamed Ould Cheikh AI-Ghazouani, Rais wa Jamuhuri ya Kiislam ya Mauritania.
Wagombea watatu wamejitokeza kuwania kiti hicho akiwemo gwiji wa siasa za Kenya, Raila Odinga.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahamoud Ali Youssouf na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Richard Randriamandrato.
Aidha, mkutano huo pia utachagua viongozi wapya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ambao ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna sita.
“Vilevile, mkutano utajadili taarifa ya ushiriki wa Umoja wa Afrika kwenye mkutano wa nchi tajiri duniani (G20),
utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na taarifa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi,” imesema
taarifa hiyo.