Samia kuongoza Kumbukumbu ya Mashujaa leo

SERIKALI imetoa mwito kwa vyombo vya habari vishirikiane na serikali kuelimisha jamii kuhusu historia ya mashujaa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema hayo baada ya kukagua maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mashujaa katika Uwanja na Mnara wa Mashujaa kwenye Mji wa Serikali, Mtumba mkoani Dodoma.

“Mshirikiane na serikali katika kuelimisha jamii kuhusu historia ya mashujaa wetu, thamani ya mchango wao, na sababu ya sisi kuendelea kuwakumbuka kila mwaka,” alisema Dk Biteko.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho leo.

Alisema siku hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuwakumbuka, kuwaenzi na kuwaheshimu mashujaa waliotoa maisha yao, nguvu zao na sadaka kwa ajili ya uhuru, amani na maendeleo ya taifa.

“Na itakuwa ni siku muhimu kwa taifa letu lakini siku muhimu katika kujenga uzalendo wa nchi yetu tunapowakumbuka mashujaa wetu ambao ndio walifanya kazi kubwa ya kuletea heshima katika nchi yetu. Kwa sababu hii tutawakumbuka mashujaa wote waliopoteza maisha yao katika uwanja wa vita waliostaafu baada ya kulitumikia taifa kwa uaminifu,” alisema Dk Biteko.

Maadhimisho hayo hupambwa na gwaride ambalo hufuatiwa na uwekaji wa zana za kivita za jadi kama ngao, mkuki, shada la maua na sime katika minara ya kumbukumbu za mashujaa.

Katika maadhimisho hayo jana saa 6 usiku, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule aliwasha Mwenge wa Kumbukumbu ya Mashujaa kwa niaba ya Rais kuashiria kuanza kwa maombolezo ya mashujaa.

Mwenge wa mashujaa utazimwa leo saa 6 usiku kuashiria hitimisho la maombolezo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa mwaka 2025.

Maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kumbukumbu ya mashujaa hufanyika kila mwaka Julai 25 kukumbuka
mashujaa waliopoteza maisha yao katika uwanja wa vita, waliostaafu baada ya kutumikia taifa kwa uaminifu
na wale waliopata majeraha katika kulinda nchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button