RAIS Samia Suluhu Hassan kesho anatarajia kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Rais Samia atazindua sera hiyo jijini Dodoma.
Msigwa alisema sera hiyo ina lengo la kuleta mageuzi katika utoaji elimu nchini na yamegusa eneo la kufundishwa somo la Tehama, mafunzo ya ufundi stadi kuanzia elimu ya msingi na matumizi ya akili mnemba.
Alisema sera hiyo imefanyiwa mapitio kuwezesha wanafunzi umahiri na ujuzi unaoakisi mahitaji kitaifa na kimataifa ili kushindana na kushiriki kikamilifu kwenye soko la ajira duniani.
Msigwa alisema sera hiyo itazalisha wanafunzi wenye maarifa, maadili na ujuzi utakaowawezesha wahitimu kwenye ngazi mbalimbali kujiajiri, kuajiri wengine na kuongeza uwezo wa ushindani kwenye soko hilo.
“Mapitio hayo yanaendana na utekelezaji wa Ilani ya CCM kuhusu kuimarisha huduma za kijamii ambapo imejielekeza kuhakikisha kila rasilimaliwatu inakuwa na ujuzi,” alisema.
Msigwa alisema mapitio hayo yameshirikisha wadau na matokeo makubwa yanatarajiwa kwa kuwa huduma ya elimu inagusa moja kwa moja jamii.
“Rais Samia alitangaza na kutoa maelekezo akitaka Wizara ya Elimu ifanye kazi kubwa ya kupitia sera na lengo lilikuwa ni kuwa na sera ambayo itawaandaa wanafunzi kuwa mahiri katika kukabiliana na changamoto za sasa na kujibu mahitaji ya dunia ya sasa,” alisema.
Alisema kuwa Rais Samia alitoa agizo hilo kwa kuwa hapendi wanafunzi wahitimu shahada wakiwa hawana ujuzi katika uzalishaji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo alisema sera hiyo itazinduliwa sambamba na vitendea kazi, ukiwamo mkakati wa utekelezaji wa sera ambao tayari umeandaliwa.
Profesa Nombo alisema sera hiyo imeelekeza kuboresha mitaala ya elimu ambayo imeboreshwa kwa ngazi zote
kuanzia ngazi ya awali na kwa upande wa vyuo vikuu uboreshaji unaendelea.
Profesa Nombo alisema mitaala iliyoboreshwa ni ya elimu ya awali, elimu ya msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la sita, elimu ya sekondari ngazi ya chini na juu na mafunzo ya ualimu.