BARAZA Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) limetangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika Baraza la Iddi.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa Bakwata Taifa, Nuhu Mruma imeeleza kuwa baraza hilo litafanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere kuanzia saa 8.30 mchana.
Mruma ameeleza kuwa sherehe za Iddi El-Fitri kitaifa zitafanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam Aprili 21 au 22 kutegemea mwandamo wa mwezi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Swala ya Iddi itaswaliwa katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI, Bakwata Makao Makuu Kinondoni kuanzia saa 1.30 asubuhi.
“Kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dk Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Mbwana anawatakia Waislamu na wananchi wote maandalizi mema ya sikukuu hiyo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.