Samia: Tujipange haki madai Dira ya 2050

Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema ni muhimu kuimarisha utoaji haki ili nchi ipate manufaa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Rais Samia amesema hayo Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria kuashiria mwanzo wa mwaka wa Mahakama.

Amesema utekelezaji wa Dira ya 2050 hautakuwa rahisi, hivyo ni vyema Mahakama na wadau waanze kujipanga.

Advertisement

Rais Samia alisema katika dira mpya sauti za wananchi wengi zinatamani miaka 25 ijayo Tanzania iwe ni taifa
jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea.

Alisema Dira ya 2050 itaweka lengo la kuongeza pato la Taifa hadi kufikia dola bilioni 700 ifikapo mwaka 2050 na ili kufikia hilo ni lazima kuchukua hatua ya kukuza sekta za kiuchumi ikiwemo kuvutia uwekezaji na biashara, kuvutia mitaji nchini na kukuza njia za ukusanyaji wa mapato nchini.

“Kufanya biashara ili kukuza uchumi mambo hayo yote yatalazimu sekta zinazohusika na haki madai kujiandaa vyema katika kutoa huduma za haki,” alisema Rais Samia.

Alisema kuongezeka kwa shughuli nyingi za kibiashara na uwekezaji zitazusha migogoro ya kisheria na uhitaji mkubwa wa huduma za utoaji wa haki.

“Haitarajiwi kwa wadau na mahakama kutumika kuchelewesha haki na badala yake tunategemea mahakama kuwa mwezeshaji wa shughuli za kiuchumi na kutenda haki kwa haraka na wakati,”alisema Rais Samia.

Aliagiza waliopewa dhamana kwenye baraza la ushauri wa kodi kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati ili wawekezaji wasicheleweshewe haki na kodi stahiki zilipwe kwa wakati.

Rais Samia alisema miaka 25 ijayo sekta ya fedha itapunguza matumizi ya fedha taslimu mkononi na kuwa na mifumo ya fedha za mitandaoni.

“Kutokana na haya ni lazima tujipange na watu wetu wanaohusika na mambo ya sheria kuangalia mambo haya, lazima tujipange vizuri,” alisema.

Rais Samia alisema kikatiba ofisi yenye dhamana na upekuzi na tathmini ya mikataba inayoingiwa na serikali na mashirika yake ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alisema katika kuhakikisha maslahi ya nchi yanaendelea kuzingatiwa kwenye mikataba itakayoingiwa ni lazima watumishi kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wawe na uwezo na ubobevu kwenye masharti ya kimikataba yanayohusu sekta za kiuchumi na uwezo wa kusimamia mikataba hiyo.

Rais Samia alisema utekelezaji wa Dira inayoishia 2025 umekuwa na matokeo chanya katika maisha ya wananchi na mabadiliko yako dhahiri katika sekta za kiuchumi, maendeleo ya jamii, sekta ya kifedha na katika sekta ya utoaji haki
na kuwepo kwa maendeleo kwenye miundombinu, vifaa na watumishi.

“Katika mahakama za Tanzania kusikilizwa kwa mashauri ama kutoa ushahidi kwa njia ya mtandao sasa ni jambo la kawaida leo hii sio simulizi tena, tulidhani haiwezekani lakini imewezekana,” alisema.

Rais Samia alisema mwaka 2024 mashauri 172,301 yalisajiliwa na kumalizika kupitia mfumo wa mtandao katika mahakama za mwanzo, mashauri 70,714 kwa ngazi ya mahakama za wilaya hadi mahakama kuu.

Alisema maboresho na mageuzi katika Mahakama ni matokeo ya mipango na hatua madhubuti kwenye mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano unaoishia mwaka 2025.

Rais Samia alisema Ilani ya uchaguzi ya CCM imeelekekeza kuimarisha Tume ya Utumishi wa Mahakama ili iweze kusimamia kwa ufanisi maadili na nidhamu katika utumishi wa mahakama.

Aidha, alisema serikali inatambua mazingira magumu ambayo watumishi wa mahakama wamekuwa wakiyafanyia kazi na akasema ni wajibu wa serikali kutengeneza mazingira mazuri na vivutio kwa watendaji wa mhimili huo.

Rais Samia alisema maombi ya kuboresha maslahi ya watumishi yanaendelea kufanyiwa kazi hatua kwa hatua na jinsi ya hali ya uchumi unavyoruhusu na akasema serikali itaendelea kuangalia maslahi ya sekta hiyo.

Aliwakumbusha majaji na mahakimu wasiwe Mungu watu, wawe upande wa haki na watende haki.

“Kuwa jaji au hakimu ni dhamana ambayo inataka uadilifu na nidhamu isitiliwe shaka hata kidogo. Kazi ya kutoa haki ni kazi ya Mwenyezi Mungu, ambaye pia ana kudra na anajalaa,” alisema Rais Samia.

Aliongeza: “Majaji na mahakimu ni mawakala wa utoaji haki hapa duniani lakini mmenyimwa kudra na jalaa, hivyo niwasihi sana, niwaombe sana tusiwe Mungu watu, tutoe haki kwa misingi ya katiba na sheria.”

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *