Samia: Tunatenda zaidi

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatenda zaidi kuliko kusema hivyo wananchi watoe ushirikiano kuongeza kasi ya maendeleo.

Alisema hayo katika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma jana alipokuwa akizungumza na wananchi akimaliza ziara mkoani humo.

“Tuna mengi ya kufanya pamoja, ongezeni jitihada jinsi serikali tunavyokuja, pokeeni, fanyeni ili Kigoma irudi kwenye historia yake ya kufanya biashara, sisi tunavipa zaidi vitendo kuliko maneno. Na tutaendelea kutenda ili sisi waja tukija mtuambie tuliyotenda,” alisema Rais Samia.

Alishukuru wananchi na wabunge kwa kusema yaliyofanywa na serikali wakati awali serikali ilikuwa inakwenda kuyasema kwa wananchi.

“Zamani sisi (serikali) ndio tuliokuwa tunasema, lakini sasa kila tunakopita ni wananchi au wabunge wanasema wenyewe miradi ya maendeleo iliyotekelezwa, hii ni fahari yetu serikali,” alisema Rais Samia.

Alisema ametembelea miradi na mingi ameifungua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi zikiwemo barabara, miradi ya maji na umeme ambayo ni kichocheo cha maendeleo mkoani humo.

Rais Samia alisema serikali ina lengo la kuiwezesha Kigoma iwe kitovu cha biashara kwa mikoa ya Magharibi na nchi jirani kwa sababu inabebwa na jiografia yake.

“Kigoma imebadilika kabisa, mara ya mwisho ilikuwa inasinzia, leo imeamka kila mahali kuna maendeleo, nimefungua umeme, nimeweka mawe ya msingi wa ujenzi wa Bandari ya Kibirizi, Hospitali ya Rufaa ya Maweni na kufungua Chuo cha Ualimu na mingine mingi, hii yote ni kuifungua Kigoma,” alisema.

Aliongeza: “Nina imani jinsi tunavyofungua Kigoma tuna uwezo wa kukusanya mapato mengi zaidi ya haya tumeanza tu yameongezeka tunavyokwenda yataongezeka zaidi.”

Rais Samia alisema ekari 142,557 zimetengwa mkoani humo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga 13,220 na wanaendelea kupangwa.

Kuhusu wadeni waliokuwa wakiidai Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Rais Samia alisema wataanza kulipwa mwisho wa mwezi huu.

Aidha, alisema serikali imetenga Sh bilioni 42 kwa ajili ya kuzalisha vitambulisho vya taifa milioni 13.

“Tuna deni la vitambulisho milioni 11 vya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ila sisi tutazalisha vitambulisho milioni 13 hivyo hata wananchi wa Kigoma waliokosa nao watapata vitambulisho vyao,” alisema Rais Samia.

Waziri wa Nishati, January Makamba alisema mikoa miwili hivi sasa haina umeme wa gridi ya taifa ukiwemo wa Katavi na Rukwa mwakani Katavi itaungwa na mwaka 2024 Rukwa.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema serikali inaendelea kujenga miundombinu ya kisasa ya barabara na reli ili Kigoma na mikoa mingine iweze kunufaika na kukua kibiashara.

“Serikali inatekeleza miradi mbalimbali Kigoma ya usafirishaji baharini na nchi kavu na tunaendelea na ujenzi wa barabara na wakandarasi wapo maeneo ya kazi na baharini tuna miradi ya chelezo kwa ajili ya ujenzi wa meli na tutatumia Sh bilioni 58.29,” alisema Profesa Mbarawa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angelah Kairuki alisema serikali imetekeleza mengi kwenye sekta ya elimu nchi nzima na kwa Mkoa wa Kigoma umepata mgao wa fedha katika Sh bilioni 160 za madarasa 8,000 nchi nzima wao wamepata madarasa 300.

Kairuki alisema katika ajira mpya mkoa huo umepata watumishi wapya 888 na katika fedha za Tarura mkoa huo umetengewa Sh bilioni 26.5.

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto alimshukuru Rais Samia na serikali kwa juhudi zinazofanywa za kuwaweka Watanzania pamoja bila kujali itikadi za vyama vya siasa.

“Nakupongeza sana kwa juhudi kubwa zinazofanyika kuwaweka Watanzania pamoja bila kujali itikadi zao, hauangalii vyama vya siasa vya watu bali unaangalia Watanzania kwa pamoja nakushukuru na kukupongeza,” alisema Zitto.

Alisema tangu Rais Samia aingie madarakani amekuwa akikutana na vyama vya siasa kimoja kimoja au kupitia kikosi kazi alichounda na sasa nchi iko tulivu.

“Ninachowaomba wana Kigoma, Rais Samia anadhamira nzuri sana sio kwa Kigoma tu bali kwa nchi, mama huyu hapa mpokeeni tufanye naye kazi tulete mabadiliko kwa nchi,” alisema

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button