Samia: Tutalinda bei za mazao

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema wananchi  wakimchagua, serikali yake italinda bei za mazao hivyo hawatayauza kwa bei ya hasara.

Samia amesema hayo kwenye mkutano wa kampeni Nakapanya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Amesema hivi sasa mbaazi na ufuta zinazalishwa wakati nchi nyingi duniani zimezalisha zao hilo.

SOMA: Samia kuongeza umeme 8000MW Namtumbo

“Kwa maana hiyo bei iliyopo duniani, hasa kwa wenzetu India ambao tunawauzia wamezalisha kwa wingi kipindi hiki. Kwa hiyo, wametushushia bei. Hata hivyo tupo nao kwenye mazungumzo,” amesema Samia.

Ameongeza: “Tunazungumza nao bei isishuke zaidi ya asilimia 60 ya bei ya mwaka jana. Tunazungumza nao, niwatie moyo kwamba bado serikali yenu inahangaikia bei ya mazao na niwahakikishie hamtauza kwa bei ya hasara.”

Samia amesema serikali inasambaza mbolea za ruzuku na pembejeo za kilimo na pia kazi ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji inaendelea, ili wakulima wazalishe mara mbili kwa mwaka.

“Natambua Nakapanya ni wazalishaji wazuri wa mazao ya kilimo. Tupo na nyinyi kwa ruzuku ya pembejeo na mbolea. Najua tumeanza kujenga mabwawa ambayo bado hayajakamilika, nayo tutakuja kuyakamilisha kwani yapo katika hatua mbalimbali,” amesema.

Samia amesema anatambua maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika eneo hilo la Nakapanya lakini bado kuna changamoto zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi.

“Hapa Nakapanya bado kuna mahitaji mengi. Nikiangalia nauona umeme na najua umefika vijiji vyote, sasa tunaunganisha kwenye vitongoji. Kuna suala la afya, najua tumejenga vituo vya afya, zahanati na ninakumbuka vyema Kijiji cha Namiungo ilikuwa tujenge kituo cha afya lakini hatukufanikiwa,”amesema.

Samia ameahidi serikali itajenga kituo hicho cha afya ili wananchi wapate huduma kwa karibu.

Pia, amesema kuna majengo ya zahanati ambayo ujenzi wake haujakamilika. Hivyo, ameahidi serikali itayamalizia.

Samia amesema bado baadhi ya maeneo yanakabiliwa na uhaba wa maji, licha ya jitihada za serikali za kufikisha huduma hiyo kwa wananchi.

“Kazi inayoendelea ni kwenda kuheshimu na kuupa hadhi utu wa mtu na ndiyo maana tunasema ‘Kazi na Utu, tunasonga mbele’. Kwa hiyo, kazi ya kusambaza maji inaendelea,” amesema.

Kwa upande wa wanyama waharibifu, Samia amesema anatambua changamoto hiyo ya wanyamapori wanaovamia mashamba.

“Natambua hapa kuna kituo kimoja tumejenga na kituo cha pili tunakijenga pale Lukumbile lakini najua kuna askari katika maeneo matano mengine. Zote hizo ni jitihada za kuwafukuza wanyama hao wasiharibu mashamba na wasiumize watu,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button