SBL yawanoa wanawake, vijana wanaosambaza vinywaji

MWANZA: Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali, Bridge for Change (BFC), imezindua programu ya  Learning for Life iliyoelenga kuwapatia wanawake na vijana wanaosambaza vinywaji Kanda ya Ziwa, ujuzi wa misingi ya biashara ili kuwa na uendelevu.

Wajasiriamali wa awali 50 walichaguliwa kutoka sehemu mbalimbali za Kanda ya Ziwa walipitia mafunzo maalumu yaliyojikita katika maeneo muhimu kama ujuzi wa biashara, elimu ya fedha, usimamizi wa mikopo na hatarishi za kifedha, usimamizi wa bidhaa (inventory management), pamoja na uongozi.

Mafunzo haya yalilenga si tu kuboresha ujuzi wa vitendo wa washiriki, bali pia kuwasaidia kukuza biashara zao kwa kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi bora ya kifedha, kuimarisha uendelevu wa biashara, na kuwawezesha kuongeza mauzo kama washirika muhimu katika mfumo wa usambazaji wa SBL.

Advertisement

Akizungumzia umuhimu wa programu hii, Gordon Katundu, Meneja wa Mauzo wa Kanda – Mwanza, kutoka SBL, alisisitiza dhamira ya kampuni katika kuchochea maendeleo jumuishi ya kiuchumi: “Katika SBL, tunaamini maendeleo ya kweli yanapimwa kwa fursa tunazozalisha kwa jamii zetu. Kupitia program ya Training for Life, tunawekeza moja kwa moja kwa wateja wetu, hususani wanawake na vijana, kwa kuwapatia ujuzi muhimu wa kukuza
biashara zao kwa njia endelevu. Hili ni jukumu la moja kwa moja katika afya ya kiuchumi ya jamii, tukiwasaidia washiriki kuimarisha biashara zao na kuleta athari chanya za muda mrefu.”

Kwa upande wake, Ocheck Msuva, Mkurugenzi Mtendaji wa BFC, alieleza manufaa halisi ya mpango huu: “Tunajivunia kushirikiana na SBL katika kuwezesha mafunzo haya yenye mchango kubwa, ambayo yanakabiliana na changamoto halisi zinazowakumba wajasiriamali.

SOMA: Mchango wa SBL kukuza usawa wa kijinsia watambulika

Maarifa yatakayopatikana katika mafunzo haya ni kama usimamizi wa biashara, usimamizi wa mikopo, usimamizi wa kifedha, masoko, na mbinu bora za uendeshaji biashara zitawawezesha washiriki kuwa na ustahimilivu zaidi, kuongeza tija, na kushindana vyema katika sekta ya usambazaji.”

Kupitia mipango ya kimkakati na ushirikiano wa kimaendeleo, SBL inaendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara kwa kuwawezesha wanawake na vijana wengi zaidi kujenga biashara endelevu za usambazaji katika jamii zao.

Mpango huu unaonesha kwa dhati jinsi SBL inavyojizatiti kuleta mabadiliko ya muda mrefu ya kijamii na kiuchumi huku ikiimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini Tanzania.
Mmoja wa wanufaika, Flora Kimathi, alishiriki uzoefu wake: “Kabla ya mafunzo haya, nilikuwa na uelewa mdogo kuhusu mienendo ya soko na usimamizi wa fedha. Sasa, nimepata mikakati ya muda mrefu itakayonisaidia kuendesha biashara yangu kwa ufanisi zaidi.”

Aliwataka vijana wajasiriamali vijana kuchangamkia fursa kama hizo kwani yanatoa maarifa muhimu yanayoweza kubadilisha biashara zao."

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *