Sekondari Enduiment yachangiwa mil 22/-
JUMUIYA ya Wanyapori ya Enduimet (WMA) wilayani Longido mkoani Arusha imechangia Sh milioni 22 na vitanda 10 kwa ajili ya mabweni mawili ya wasichana ya shule ya Sekondari ya Enduimet iliyopo Longido yaliyoungua moto mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Shule hiyo iliyopo kijiji cha Lerangwa kata ya Olmology tarafa ya Enduiment Longido, mabweni mawili yaliungua moto usiku wa Agosti 26 mwaka huu hata hivyo chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.
Akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo, Makamu Mwenyekiti wa WMA, Peter Lekanet ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido amesema kiasi hicho cha pesa ni kufuatia michango ya Sh milioni 2 kwa vijiji 11 vya tarafa ya Enduimet.
SOMA: Waiomba serikali kujenga uzio shule za serikali
Lekanet amesema pamoja na mchango huo utakaosaidia ununuzi wa vitanda,magodoro na blanketi pia vijiji hivyo vimetoa msaada wa vitanda 10 kwa shule hiyo kwa ajili ya wanafunzi ambao bado wanauhitaji Kwa sababu wanafunzi bado wanalala chini baada ya vitanda vya awali,magodoro na blanket vyote kuungua moto.
Makamu Mwenyekiti wa WMA na Halmashauri ya Longido aliwaomba wadau mbalimbali wa elimu na Maendeleo Longido kujitoa katika kuwasaidia wanafunzi hao kwani mahitaji ya wanafunzi ni makubwa na kumwachia Mbunge wa Jimbo la Longido na Naibu Waziri wa Madini,Dk Steven Kiruswa pekee yake sio sawa kwani wanafunzi wanaosoma shule hiyo ni wa ndani ya Longido na nje.
Mke wa Kiruswa, Agnes Kiruswa akikabidhi magodoro 80 na blanketi 100 na vichujia maji vinane kwa niaba ya mbunge alisema malengo ya Mbunge bado hayajatimia hivyo amekabidhi kiasi ili kutimiza malengo ya magodoro 485 na blanketi za kiasi hicho kwa mabweni mawili ya wasichana ya shule hiyo.
Amesema mbunge kama alivyoahidi atafanya hivyo ila wasichana nao wanapaswa kusoma na kufanya vema katika mitihani ya Kitaifa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuacha mara moja mambo yasiyokuwa ya msingi kwani yanaweza kurudisha nyuma malengo yaliyokusudiwa.
Makamu mkuu wa shule hiyo, mwalimu Williamu Mangochi amemshukuru Kiruswa kwa moyo wa kujitoa na kumwomba kuendelea na moyo huo.
Mwalimu Mangochi aliwaomba wadau wengine kuiga mfano wa mbunge kwani shule hiyo sio ya Mbunge pekee yake bali ni ya wazazi wa Longido na nje ya Longido hivyo wadau wote wa maendeleo Longido wanapaswa kujitoa kwa hali na mali kuwasaidia wanafunzi hao kulala sehemu salama.