Sekta binafsi kuchangia tril 60/- Mpango wa Maendeleo

SERIKALI imesema sekta binafsi inatarajiwa kuchangia Sh trilioni 60.1 katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2026/2027 ambazo ni sawa na asilimia 69.6 ya kiasi kitakachotumika.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema hayo wakati akiwasilisha kwa wabunge mapendekezo ya serikali ya mpango huo Dodoma jana.
Profesa Kitila alisema Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/2027 unatarajiwa kutekelezwa na wadau wakubwa watatu ambao ni Serikali Kuu na mamlaka za serikali za mitaa, sekta binafsi na mashirika ya umma.
Alisema katika utekelezaji huo, sekta ya umma kwa ujumla wake inatarajiwa kuchangia Sh trilioni 26.2 (sawa na asilimia 30.4) na mashirika ya umma yanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 5.5.
Alisema serikali itachangia Sh trilioni 20.7 itakayotengwa kutoka katika Bajeti Kuu ya Serikali ya Sh trilioni 62.3 na kwamba kiasi hicho ni sawa na asilimia 33.3 ya bajeti hiyo.
Profesa Kitila alisema mchango wa sekta binafsi unatarajiwa kupatikana kupitia uwekezaji katika ukuzaji wa mitaji, hususani katika mali za kudumu na shughuli za kiuchumi na kijamii.
Alitaja shughuli hizo kuwa ni viwanda na biashara, nishati na madini, kilimo, mifugo na uvuvi, maji, afya, elimu, utalii, mitambo, mashine, miundombinu ya uzalishaji, miundombinu ya usafiri na usafirishaji na teknolojia.
Profesa Kitila alisema gharama za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2026/2027 zinakadiriwa kuwa Sh trilioni 86.3 (sawa na asilimia 18.1 ya gharama za kutekeleza Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano).
Gharama ya kutekeleza Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ili kufikia malengo yaliyowekwa, inakadiriwa kuwa Sh trilioni 477.747.
Aliwaeleza wabunge kwamba kati ya fedha hizo asilimia 70 (trilioni 324.487) inatarajiwa kutoka katika sekta binafsi na asilimia 30 (trilioni 153.26) kutoka katika sekta ya umma (Serikali Kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma).
Profesa Kitila alisema katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/2027, serikali inapendekeza kutekeleza maeneo matano ya kipaumbele kama yalivyoainishwa katika Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni kuimarisha utawala bora, demokrasia, amani na utulivu, kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani na kuimarisha uwezo wa watu na maendeleo ya jamii.
Profesa Kitila alitaja maeneo mengine kuwa ni kuimarisha uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu kwa mabadiliko ya tabianchi na vichocheo vya mageuzi ikiwemo nishati, miundombinu ya usafiri na usafirishaji, utafiti na maendeleo na mageuzi ya kidijiti.
Alisema serikali imepanga kutekeleza programu na miradi 408, ikiwemo miradi shikizi 38 iliyopo katika programu saba za kielelezo zilizoainishwa katika Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Profesa Kitila alisema mashirika ya umma yanatarajiwa kutekeleza programu na miradi itakayopunguza ruzuku kutoka serikalini na kupunguza hasara, kuanzisha hatifungani za kampuni, kuthaminisha rasilimali, kuunganisha baadhi ya mashirika ya umma ili kuongeza ufanisi na kuwezesha mashirika ya umma kuingia katika masoko ya hisa ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika kukuza mitaji.
Aidha, mashirika ya umma yanatarajiwa kuwekeza katika sekta mbalimbali, zikiwemo za nishati, usafiri na usafirishaji, kilimo, afya, miliki, utalii, mawasiliano, madini, huduma na uzalishaji viwandani.
Matarajio
Profesa Kitila alitaja yanayotarajiwa kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa mwaka 2026/2027 kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa ajira kufikia milioni 1.7 mwaka 2026/2027 ikilinganishwa na ajira 981,000 zilizozalishwa mwaka 2024/2025 katika sekta za kilimo, uzalishaji viwandani na huduma hususani utalii, biashara na usafiri.
Alitaja matarajio mengine kuwa ni kuongezeka kwa mapato ya kodi kufikia asilimia 13.7 ya Pato la Taifa na kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa pato hilo kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026.
Matarajio mengine ni kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme kufikia megawati 4,654.5, ikilinganishwa na megawati 4,504.54 mwaka 2025/2026 na mfumuko wa bei kuendelea kuwa katika wigo wa asilimia tatu hadi tano.
Alitaja mengine kuwa ni kuongezeka kwa eneo la umwagiliaji kufikia hekta milioni 1.2 (ikilinganishwa na hekta 980,000 mwaka 2024/2025) na kuongezeka kwa mizigo inayosafirishwa katika reli kufikia tani 810,000, ikilinganishwa na tani 531,359 mwaka 2024/2025.



