Sekta ya utalii Tanzania ‘imepaa chini ya mikono’ ya Rais Samia

SEKTA ya utalii nchini Tanzania imeendelea kupata mafanikio makubwa mwaka 2024, jambo linalodhihirisha namna ambavyo juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan zilivyozaa matunda ya kweli.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa na Rais Samia wakati akihitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Juni 27, 2025 idadi ya watalii wa kimataifa waliotembelea Tanzania imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia 2,141,895 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 132.1.

Aidha, idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka 788,933 hadi 3,218,352 kwa mwaka 2024, ongezeko la asilimia 307.9. Takwimu hizi si tu kwamba zinaashiria mafanikio ya kampeni za utalii, bali pia zinadhihirisha jinsi taswira ya Tanzania ilivyoboreshwa kimataifa kama moja ya nchi salama, zenye vivutio vya kipekee na vya kimkakati katika Afrika.

Ufanisi filamu ya The Royal Tour Moja ya sababu kubwa ya mafanikio haya ni uzinduzi wa filamu ya ‘Tanzania: The Royal Tour’, iliyomshirikisha Rais Samia mwenyewe akiwa kama mwongozaji wa vivutio vya nchi. Filamu hiyo ilizinduliwa Aprili 2022, nchini Marekani na baadaye kusambazwa katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa kama ndege za kimataifa, runinga za nje na majukwaa ya kidigiti.

Kupitia filamu hiyo, watazamaji wa kimataifa walivutiwa na maeneo kama Mlima Kilimanjaro, Bonde la Ngorongoro, Serengeti, Mji Mkongwe wa Zanzibar, pamoja na fukwe nzuri za Bahari ya Hindi. Filamu hiyo pia imefungua milango ya utalii kutoka masoko mapya ambayo hayakuwahi kushamiri hapo awali, ikiwemo China, Urusi, Poland na Israel.

“Hii filamu si tu imeitangaza Tanzania, bali imetufungulia soko la kiutalii la dunia kwa namna ambayo hatujawahi kushuhudia,” anasema mmoja wa maofisa waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwa upande wa ndani, The Royal Tour imewaamsha Watanzania wengi waliokuwa hawajawahi kufikiria kutembelea vivutio vya ndani ya nchi.

Kampeni za kuhamasisha utalii wa ndani zimekuwa na mafanikio makubwa, hasa kutokana na kuimarika kwa miundombinu na urahisi wa upatikanaji wa huduma. Miundombinu bora yachochea mafanikio Serikali kupitia wizara na taasisi zake mbalimbali imeboresha miundombinu inayosaidia ukuaji wa utalii.

Barabara zinazounganisha mbuga za wanyama na vivutio vingine zimekarabatiwa, viwanja vya ndege vidogo kama vile Saadani vimeboreshwa, na huduma za malazi ya watalii, ikiwa ni pamoja na hoteli, loji na kambi za muda zimeongezeka na kuboreshwa.

Uboreshaji huo umesaidia kuondoa vikwazo vya usafiri na usafirishaji, hali iliyosaidia watalii wa ndani na wa kimataifa kufika kwa urahisi kwenye vivutio.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeripoti ongezeko la watalii waliotembelea misitu ya asili kutoka 55,427 mwaka 2019 hadi zaidi ya 250,000 mwaka 2024, ishara ya mafanikio ya juhudi hizi. Ushirikiano wa kimataifa na wadau wa ndani Serikali pia imekuwa na ushirikiano wa karibu na taasisi za kimataifa kama Shirika
la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na mashirika ya ndani kama Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), TFS na wadau binafsi katika sekta hiyo.

Kupitia ushirikiano huu, Serikali imetoa mafunzo kwa wahudumu wa utalii, imeimarisha uhifadhi wa mazingira pamoja na kubuni mbinu bunifu za kutangaza vivutio vya Tanzania kwa ufanisi zaidi.

Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Maliasili kwa Utalii na Ukuaji (REGROW) unaotekelezwa Kusini mwa Tanzania kwa usaidizi wa Benki ya Dunia ni mfano bora wa miradi ya kimkakati inayoleta matokeo chanya. Faida za kiuchumi Kwa sasa sekta ya utalii nchini ni moja ya nguzo muhimu za uchumi wa taifa.

Mwaka 2023 pekee, sekta hiyo ilichangia asilimia 17.2 ya pato la taifa, huku mapato yatokanayo na utalii yakifikia Dola za Marekani bilioni 3.4 sawa na ongezeko la asilimia 31 ukilinganisha na miaka ya nyuma. Zaidi ya mapato ya Serikali, ongezeko la watalii limekuwa kichocheo kikubwa cha ajira hasa kwa vijana katika maeneo ya vijijini.

Watoa huduma za usafirishaji, wauzaji wa bidhaa za mikono, wamiliki wa malazi, waongozaji watalii na waendesha bodaboda wamekuwa miongoni mwa wanaonufaika wa moja kwa moja na sekta hiyo. “Hawa watalii wanatuletea fedha vijijini. Sisi tumeanza kuuza hata vyakula vya asili kama sehemu ya kuvutia wageni,” anasema mmoja wa wakazi wa Karatu anayejihusisha na utalii wa kijijini.

Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mwanza, Mbeya na Zanzibar imeendelea kuwa kitovu cha ongezeko la shughuli za kiutalii na uchumi linalotokana na wageni wa ndani na wa nje. Tuzo zazidi kuimarisha taswira ya Tanzania Mafanikio hayo yamepata msukumo zaidi kufuatia ushindi wa tuzo 27 za kimataifa za utalii zilizotwaliwa na Tanzania hivi karibuni.

Tuzo hizo zimeimarisha hadhi ya Tanzania kimataifa na kutoa mvuto mpya kwa watalii wanaotafuta vivutio vya kipekee barani Afrika. Ushindi wa tuzo 27 kimataifa unaakisi ubora wa vivutio, huduma na mikakati ya utangazaji ya Tanzania.

Tanapa imeongoza kwa kujinyakulia tuzo 7, ikiwa ni pamoja na ‘Shirika Bora la Usimamizi wa Hifadhi za Taifa Afrika’ na ‘Ubunifu wa Utalii wa Asili.’ Bonde la Ngorongoro, moja ya vivutio vya kipekee duniani, limetambuliwa kama moja ya ‘Maeneo 10 Bora ya Utalii wa Mandhari Asilia Afrika,’ huku Serengeti ikitunukiwa tuzo ya ‘Hifadhi Bora Barani Afrika kwa Mwaka wa Pili Mfululizo.’

Mlima Kilimanjaro pia umetajwa kuwa miongoni mwa ‘Vivutio Bora vya Kupanda Milima Duniani.’ Fukwe za Zanzibar, Mji Mkongwe pamoja na Hifadhi ya Ruaha na Mikumi zimechangia idadi hiyo ya tuzo, huku baadhi ya loji na hoteli binafsi zikitambuliwa kwa ubora wa huduma, mazingira rafiki na mchango katika utalii endelevu.

Ni wazi kuwa ushindi huu umefungua milango zaidi kwa watalii kutoka soko la kimataifa na kuongeza imani ya wawekezaji katika sekta ya utalii nchini. Bado kuna changamoto Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kadhaa bado zinakabili sekta ya utalii nchini.

Gharama za juu za safari, utoaji wa huduma usioridhisha katika baadhi ya maeneo pamoja na ushindani kutoka nchi jirani kama Kenya na Rwanda, ni baadhi ya masuala yanayohitaji kushughulikiwa kwa haraka. Aidha, baadhi ya vivutio havijafikika kwa urahisi kutokana na changamoto za miundombinu au ukosefu wa matangazo ya kutosha.

Wapo watalii waliotembelea mara moja lakini hawakurudi tena kutokana na huduma duni walizozipata katika baadhi ya maeneo. Serikali imeweka mikakati ya kuboresha hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kupunguza kodi kwa wawekezaji wa sekta ya utalii, kuimarisha usalama wa watalii na kuongeza uwazi wa gharama kwa watalii wa ndani.

Malengo ya baadaye Kwa mujibu wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, serikali inalenga kufikia idadi ya watalii milioni 5 na mapato ya Dola za Marekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025. Ili kufanikisha hilo, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mipya ikiwemo kutangaza vivutio vipya, kukuza utalii wa kihistoria, kiutamaduni, kiikolojia na utalii wa mikutano.

Pia, jitihada za kuhamasisha Watanzania kushiriki katika sekta ya utalii kama wamiliki wa biashara ndogo ndogo, waongozaji watalii na wawekezaji wadogo zinaendelea kwa kasi. Serikali pia imeelekeza nguvu kuboresha data na takwimu za utalii ili kusaidia mipango ya kisera. Ongezeko la watalii mwaka 2024 linaonesha wazi kuwa sekta ya utalii nchini imeingia katika hatua mpya ya ukuaji.

Kwa asilimia 132.1 ya ongezeko la watalii wa kimataifa na asilimia 307.9 kwa wa ndani, Tanzania inaelekea kuwa miongoni mwa nchi vinara wa utalii barani Afrika. Kupitia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, sekta hii imepata msukumo mpya ambao haujawahi kushuhudiwa.

Ikiwa juhudi hizi zitaendelezwa, Tanzania inaweza kujijengea msingi thabiti wa utalii endelevu na shirikishi unaochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Watanzania wote.

Mwandishi ni msomaji na mchangiaji katika gazeti hili.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button