Selous; Hifadhi ya kipekee kwa uwindaji wa kitalii

PORI la Akiba la Selous linapatikana katika mikoa miwili ya Pwani wilayani Rufiji na Mkoa wa Lindi katika wilaya za Kilwa na Liwale.

Pori hilo ambalo ni Urithi wa Dunia wa Asili liko chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Kanda ya Kusini Mashariki.

Katika mazungumzo na HabariLEO Ikwiriri wilayani Rufiji, Ofisa Utalii Hifadhi ya Wanyamapori Selous, Stephano Lukumay anasema, “Ingawa hili ni Pori la Akiba la Selous, sisi tunapenda kuliita Hifadhi ya Wanyamapori ya Selous ambayo kimsingi, ndiyo pori kongwe kuliko mapori yote Tanzania.”

Anasema hifadhi hiyo iliyoko Kusini Mashariki mwa Tanzania, ina ukubwa wa kilometa za mraba 18,020.
Anasema hifadhi hiyo ina ina utajiri mkubwa wa aina mbalimbali za wanyamapori na bayoanuai na kuongeza kuwa ni eneo bora kwa utalii wa uwindaji hasa kutokana na uwepo wa aina nyingi za wanyamapori.

“…Selous ina jumla ya vitalu 15 na matumizi ya hivi vitalu kwa sasa ni uwindaji wa utalii pekee na miongoni mwa hivyo vitalu hivyo, vyenye wawekezaji ni 12,” anasema Lukumay.

Anasema matumizi ya vitalu hivyo yamegawanyika katika matumizi ya aina mbili, ambayo ni matumizi ya uwindaji wa kawaida yaliyochukuliwa na vitalu 10 pamoja na matumizi mseto yaliyochukuliwa na vitalu vitano.

Katika matumizi ya uwindaji wa kawaida, mwekezaji anapewa kitalu kwa miaka 10 na ataruhusiwa kufanya utalii wa uwindaji pekee.

Kwamba, mwekezaji huyo haruhusiwi kufanya shughuli nyingine zozote za utalii lakini katika matumzi mseto mwekezaji anapewa kitalu kwa miaka 20 hadi 30 na anaruhusiwa kufanya utalii wa uwindaji pamoja na utalii wa picha.

Lukumay anasema kwa sasa vitalu vyote 10 vya uwindaji wa kawaida vimeshapata wawekezaji na vile vya matumizi mseto ni vitalu vitatu ndiyo vyenye wawekezaji.

“Katika vitalu mseto, watu wanakuja kufanya utalii wa picha lakini kinachotuongoza ni lini tunafanya utalii wa picha, ni mpango wa biashara wa mwekezaji,” anasema.

Anaongeza: “Kwa sasa vimechukuliwa vitalu viwili vya matumizi mseto. Mwaka 2023 kitalu cha kwanza kilichukuliwa na cha pili kimechukuliwa mwaka huu 2025 na ndiyo tunaanza kupata uwekezaji katika utalii mseto.”

Anasema kwa Selous unapotaka kuzungumzia vivutio vya utalii, ndipo linapokuja suala la vitalu vya matumizi mseto ambayo ndani yake, kuna vivutio vinavyoweza kutembelewa kwa utalii wa picha.

Hata hivyo anasema utalii wa picha unafanyika kwa makubaliano ya mtalii na mmiliki wa kitalu chini ya kanuni zilizowekwa na Tawa kwa mujibu wa sheria.

Anasema watalii wanapaswa kulipa tozo zilizowekwa na mamlaka hiyo, ikiwa ni nje ya malipo watakayokubaliana na mmiliki wa kitalu husika.

Anasema utalii wa picha unaweza kufanyika msimu usio na shughuli za utalii wa uwindaji zinazoendelea.
“…Huwezi kupeleka mtu akapige picha maana kule ni kulenga shabaha; ni risasi tu zinarindima, lakini sheria zinafuatwa kwa wale wanaowinda. Haiwezekani watu wanawinda halafu mtu aende kwa utalii wa kupiga picha,” anasema.

Anafafanua: “Isipokuwa, kuna msimu kama huu wa masika mvua zinanyesha uwindaji hauwezi kufanyika… waayama wanajificha, majani ni marefu, kumuona mnyama huwezi kwa hiyo kipindi hiki hawafanyi.

“Kwa hiyo kama ni hilo eneo lingine la matumizi mseto, kwa utalii wa picha ingewezekana kama barabara za kwenye vitalu zingefaa kwa mazingira haya ya sasa ingewezekana kufanya utalii wa picha”.

Akizungumzia vivutio vinavyoweza kutumika kwa utalii wa picha kwenye vitalu vya matumizi mseto ndani ya Selous, Lukumay anasema kuna utajiri wa aina mbalimbali za wanyamapori na vivutio vingine vingi.

Anasema: “Katika wanyama hao, kuna wale waliowekewa umakini wa kipekee kama vile mbwa mwitu; sehemu kubwa ya Selous ina mbwamwitu wengi sana.

“Kwa Tanzania inaweza ikawa ni miongoni mwa hifadhi ambayo ina mbwamwitu wengi zaidi kuliko hifadhi nyingine japo kwenye hali ya dunia wako hatarini kutoweka.”

Jiwe la Obasi na Jiwe la Chema
Lukumay anasema hayo ni mawe mawili makubwa yaliyo ndani ya Selous yaliyotumika kama maficho ya Wajerumani katika Vita ya Pili ya Dunia mwaka 1939 mpaka 1945. Mawe hayo pia, yalitumika kama mnara kuwaona maadui kabla hawajafika eneo hilo.

Anasema vivutio vingine ni vilima vya Nandanga na Luhombero vinavyomwezesha mtalii kuona eneo kubwa la Selous anapopanda juu yake.

Ipo pia, mito inayotitirika katika hifadhi hiyo kukamilisha mandhari nzuri na ya kuvutia sambamba na kutoa fursa ya makazi kwa viumbe wa majini kama viboko na wale waishio pembezoni mwa mito wakiwemo ndege wa aina mbalimbali, chui na aina mbalimbali za nyani.

“Kivutio kingine ni mito inayotiririka katika hifadhi hiyo ikiwemo Mto Matandu, Lung’onya, Lukulilo, Mkindu, Mbarang’andu, Mliwasi na Mto Rufiji. Hii ni mito ambayo kimsingi ndani unaweza kukutana na viumbe wanaoishi majini kama mamba, samaki viboko na ndege wa majini,” anasema.

Sambamba na hayo, hifadhi hiyo imepambwa na misitu ya Tundu, Lukwulilo, Liwande, Nyakisiku na Liuni na kutandikwa na uwanda wa nyasi tambarare na uwanda wa miombo unaotengeneza hali ya utulivu yenye kuvutia.

Shule ya Nyakisiku
Lukumay anasema pamoja na vivutio vya viumbepori pia, kuna vivutio vya kihistoria ndani ya Selous, ikiwemo magofu ya Shule ya Nyakisiku anayosema ndiyo aliyosoma mwanaharakati wa ukombozi wa Tanganyika, Bibi Titi Mohamed pamoja na miti iliyogeuka kuwa mawe.

“Kuna miti iliyogeuka mawe baada ya kukaa muda mrefu sana lakini awali ilikuwa miti, baada ya kuanguka na kukaa kwa miaka mingi ikageuka mawe na inasemekana miti hii imechukua zaidi ya miaka milioni moja kugeuka mawe,” anasema.

Fursa za kiuchumi na uwekezaji
“Kwa sasa, kwanza ni vitalu ambavyo havina uwekezaji, vile vitatu. Zile tayari ni fursa za kiuchumi kwa maana kwamba havitumiki na vinatakiwa kutumika kwa wawekezaji watakaokuja kuwekeza,” anasema Lukumay alipozungumzia fursa za uwekezaji zinazopatikana katika hifadhi ya Selous.

Anasema mwekezaji katika vitalu anafaidika kwa kuuza wanyama wanaowindwa wakati wa utalii kadiri ya mpango wake wa biashara na mwongozo wa kibali alichopewa kisheria.

Anataja uwekezaji mwingine kuwa ni kusafari kwa kutumia maputo katika maeneo ya vitalu vya matumizi mseto.

“Wale wenye vitalu vya matumizi mseto, kuna baadhi ya vitalu vina uwanda wa tambarare ambao kimsingi maana yake ni eneo la wazi ambalo huyu mwekezaji anaweza akaanzisha safari za kutumia Maputo na watalii wakafurahia.

“Anaweza kualika makampuni mengine, lakini lazima kufuata kanuni za Tawa,” anasema.

Ushuhuda wa watalii
Baadhi ya watalii wanaeleza uzoefu wao na kile walichokiona wakati wa utalii wa uwindaji ndani ya Mbuga ya Selous na kuonesha kuvutiwa na utalii walioufanya siku za karibuni.

David Daniel kutoka Texas nchini Marekani anasema, “Hii ni mara yangu ya kwanza kutembelea hifadhi za Afrika. Nimekuwa hapa kwa siku 14. Huu umekuwa wakati mzuri sana kuwa hapa.

“Nikiwa hapa nimefanikiwa kuona nyati, nyani na hata pundamilia. Kwa kweli mimi na wenzangu hapa tumekuwa na wakati mzuri sana hapa Tanzania maana hata chakula ni kizuri sana… Ni wakati wetu kuondoka lakini lazima tutarudi tena.”

Mtalii huyo, Mmarekani anawapongeza maofisa wa Tawa kwa ushirikiano waliowapa kiasi cha kuwafanya wafurahie utalii wa uwindaji katika hifadhi hiyo.

Naye, Sybrand Coetzee, raia wa Namibia anasema hakutarajia kufanya utalii kwa namna ya kuvutia kama alivyofanya katika Hifadhi ya Selous.

Anasema, “Hii ni mara ya kwanza kutembelea Selous, Tanzania. Mazingira na mandhari inavutia, tumefanya uwindaji kwenye maeneo mengi ya Afrika, lakini eneo hili ni la kipekee.

“…Kwa kweli ni bahati kubwa kwetu kuwa hapa, tunaweza kusema asante sana kwa kila mtu hapa, tuna madereva wa ajabu, hata sikufikiria kama wangetuwezesha kupata hawa wanyama”.

Anaongeza: “Kwa kweli tunajiona wenye bahati na tutapendekeza kwa wengine watembelee Selous.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button