SENSA2022: DC aridhishwa na zoezi la Sensa Mpanda

MKUU wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf akihesabiwa

MKUU wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf amesema hadi mchana wa leo zoezi la Sensa linaendelea vizuri katika Wilaya hiyo.

DC Jamila ameiambia HabariLEO mara baada ya kuhesabiwa kuwa, pamoja na kuwa zoezi hilo limeanza leo hakuna changamoto zozote zilizo ripotiwa.

“Hatujapata changamoto, makarani ambao walionyesha utovu wa nidhamu walianza kuchukuliwa hatua mapema kabisa wakati wako kwenye mafunzo, sisi hatuna karani ambaye ameshamaliza mafunzo halafu ana matatizo, kwa Wilaya ya Mpanda hiyo hatuna”

Advertisement

Karani wa Sensa Kata ya Ilembo yalipo makazi ya Mkuu huyo wa Wilaya, Emile Kimambo amesema zoezi hilo linahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa wananchi ili zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda,Haidary Sumry mara baada ya kuhesabiwa amesema zoezi la kuhesabu awamu hii liko tofauti na miaka ya nyuma kwani maswali yanayoulizwa hakika yanalenga kutatua changamoto za wananchi.

“Yapo maswali ya maji,namna wanachi tunavyopata huduma za maji,maji tunayapata kwenye maeneo gani,ni maswali ambayo unaona kabisa yanalenga kujua ukubwa wa tatizo au ukubwa wa mafanikio” alisema Haidary Sumry, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda.