Serikali, Costech, CRDB kuwapa wabunifu mikopo nafuu

SERIKALI imetenga Sh bilioni 2.3 kwa ajili ya mikopo nafuu kwa vijana wabunifu na watafiti nchini, ikiwa ni hatua madhubuti ya kuikuza sekta ya ubunifu na teknolojia.

Mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) na Benki ya CRDB kupitia CRDB Foundation, ambapo mikopo hiyo inalenga wabunifu walioko kwenye hatua za mwisho za kuingiza bidhaa na huduma sokoni lakini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji.

Akizungumza Dar es Salaam jana Aprili 17,2025 wakati wa hafla ya utiaji saini kati ya CRDB Foundation na COSTECH iliyofanyika, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za serikali kuwezesha bunifu zenye tija kuingia katika mnyororo wa thamani wa kiuchumi.

“Serikali imejipanga kuinua bunifu zinazoweza kuchangia uchumi kwa kuzisaidia kuingia kwenye mnyororo wa thamani na kuleta matokeo chanya kwa taifa,” amesema Profesa Mkenda.

Mkenda amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wizara imetenga kiasi cha Sh bilioni 5 kwa ajili ya kuipatia COSTECH ili iweze kusomesha vijana wanaomaliza kidato cha sita kuhusu akili mnemba pamoja na Sayansi ilikusaidia nchi kwenda na teknolojia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, dk Amos Nungu alibainisha kuwa mkopo huo utawanufaisha moja kwa moja wabunifu waliothibitisha uwezo wa kuzalisha bidhaa au huduma zenye tija kwa jamii.

“Tunawapa kipaumbele wabunifu ambao tayari wana bidhaa au huduma zenye tija lakini wanakosa mtaji wa mwisho ili kuingia sokoni. Lengo ni kukuza ubunifu wa ndani na kusaidia juhudi za serikali za kuujenga uchumi wa viwanda kupitia teknolojia na ubunifu,” amesema Dk Nungu.Amesema mkataba huo ni muendelezo wa juhudi zilizozinduliwa mwaka 2023, kwa lengo la kusaidia vijana kuanzisha na kukuza biashara kupitia programu ya IMBEJU BUNI.

“Tutahakikisha kuwa vijana wanapata mazingira bora ya kuibua na kukuza mawazo yao ya kibunifu, pamoja na huduma za ushauri na mafunzo yanayohitajika kwa mafanikio ya biashara zao,” amesema Nungu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB Foundation, Tully Mwambapa, amesema kuwa ushirikiano huo unaendana na dhamira ya CRDB ya kujenga uchumi jumuishi unaowajumuisha vijana na wanawake, hasa waliopo pembezoni mwa mfumo rasmi wa kifedha.

“Kupitia IMBEJU, tumelenga kuwafikia vijana waliokosa fursa rasmi za kifedha. Kupitia mkataba huu mpya, tunatarajia kuwafikia vijana zaidi ya 1,000 kwa kuwapatia mitaji, mafunzo ya ujasiriamali, na elimu ya fedha,” amesema Mwambapa.

Takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa, zaidi ya vijana 700 wabunifu wamewezeshwa kupitia dirisha la IMBEJU BUNI, na jumla ya mitaji yenye thamani ya shilingi bilioni 5 imetolewa kwa ajili ya kukuza biashara zao.

Hatua hiyo inaonesha dhamira ya kweli ya Tanzania katika kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya ubunifu na ujasiriamali wa vijana, huku sekta ya fedha na teknolojia zikishirikiana kwa karibu kufanikisha ndoto za kizazi kipya cha wajasiriamali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button