Serikali, GATSBY Africa wajadili malengo Dira 2050

SERIKALI na GATSBY Africa wamejadiliana vipaumbele vya Tanzania katika mabadiliko ya kiuchumi hasa katika kuimarisha ushindani wa uzalishaji wa viwanda ili kufi kia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa GATSBY Africa, Justin Highstead aliyeambatana na wajumbe wengine kutoka taasisi hiyo.
Balozi Omar amesema majadiliano hayo yanalenga vipaumbele vya nchi ambavyo vimeainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano na vinapaswa kutekelezwa ili kufikia lengo la taifa.
“Hapa katikati katika utekelezaji Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Mpango wa Maendeleo, tumeangalia kwa pamoja, mageuzi ya kiuchumi kwanza ambapo ndani yake kuna ya mapinduzi ya viwanda, uwekezaji mkubwa wa kifedha pamoja na uwekezaji mkubwa wa kujenga rasilimaliwatu,” alisema Balozi Omar.
Ameongeza kuwa katika kikao hicho walijadiliana pia masuala ya sayansi na teknolojia, utafiti pamoja na utafutaji wa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele hivyo ambako baadaye wataangalia namna bora ya kushirikiana katika utekelezaji. SOMA: Atoa maagizo vituo uwezeshaji wananchi kiuchumi
Aidha, ameipongeza taasisi hiyo kwa ushirikiano ambao imekuwa ikitoa hususani ushirikiano na Tume ya Mipango katika kuandaa tafiti na uchambuzi unaosaidia utekelezaji wa dira na mipango ya maendeleo ya taifa na maendeleo ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa GATSBY Africa, Justin Highstead alisema taasisi hiyo inafanya kazi Afrika Mashariki kwa ujumla hasa Tanzania kwa zaidi ya miaka 25 na inalenga mageuzi ya kiuchumi na kusaidia mabadiliko ya sekta mbalimbali za uchumi.
Highstead amesema kazi wanazofanya zinahusisha ushirikiano wa karibu na serikali, pamoja na sekta binafsi ili kusaidia juhudi za serikali katika kukuza uchumi na kuendeleza sekta zenye uwezo wa kubadilishana uchumi wa nchi.



