DAR ES SALAAM: KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kupitia kwa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja (PBPA) kuufanyia maboresho mfumo wa SCADA.
Mfumo huo umebuniwa kwa lengo la kudhibiti changamoto ya upotevu wa mafuta yanayoingizwa nchini.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyejikiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mathayo David wakati wa ziara ya kutembelea miundombinu inayotumika kupakua na kuhifadhi mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mathayo amesema kuwa mfumo wa Supervisory Control And Data Acquisition (SCADA) uendelee kufanyiwa maboresho ili lengo la kuanzishwa kwake lifikiwe kama Serikali ilivyokusudia katika masuala ya udhibiti na usalama wa mafuta pamoja na utunzaji wa kumbukumbu muhimu za mafuta.
“Umiliki wa mfumo wa SCADA uwe chini ya Serikali mara baada ya mkataba wa mkandarasi aliyefunga mfumo huo kumalizika, sio tena kubakia kwa mkandarasi ili kuweza kuimarisha ulinzi katika mfumo huo.” Amesema Mathayo
Kamati imeshauri kuwa flowmeter zote zilizopo Bandari ya Dar es Salaam ziwekewe uzio pamoja na kufunga kamera za kisasa (CCTV camera) kwa sababu zinasaidia kutazama usalama wa Nchi kwenye masuala ya mafuta ikiwemo udhibiti na ubora wa mafuta.
Amesema kampuni ya Tiper itazame uwezekano wa kupunguza gharama ya kuhifadhi mafuta kwenye matenki yake, jambo litakalosaidia kuwapunguzia gharama wafanyabishara wadogo wanaotumia miundombinu ya Tiper kuhifadhi mafuta yao.