Serikali imejizatiti mazingira bora watumishi

TANGA; Serikali imesema itaendelea kuboresha maslahi ya watumish, ikiwemo makazi bora kwa lengo la kuongeza tija katika utoaji huduma kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni pamoja na nyumba tatu za wakuu wa idara.
Amesema kuwa ujenzi wa miradi hiyo ya makazi kwa watumishi ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma.

” Niwapongeze halmashauri kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi hiyo, lakini muhimu kuzingatia usimamia mzuri ili thamani halisi ya fedha ambayo imetumika iweze kuonekana,”amesema Nyamwese.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, amesema kuwa miradi hiyo inalenga kuwezesha viongozi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kwa kuwa na makazi ya karibu na maeneo ya kazi.

”Utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea kwa mujibu wa ratiba na viwango vilivyopangwa na usimamizi thabiti unahitajika ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa ubora unaotarajiwa,”amesema.



