Serikali kuimarisha huduma kwa watoto wachanga

DAR ES SALAAM: SERIKALI imeeleza kuwa itatumia matokeo ya utafiti kuhusu huduma kwa watoto wachanga kuimarisha huduma za afya, kuboresha usaidizi wa unyonyeshaji na kuzuia maambukizi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua Kongamano la 18 la Utafiti la Chuo Kikuu lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Alisema Wizara ya Afya itatumia matokeo ya utafiti huo kupitia miongozo ya huduma kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati na wenye uzito mdogo, ambao wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi, changamoto za kunyonya na kupoteza joto la mwili.
Dk Magembe alisema vifo vya watoto wachanga bado ni changamoto kubwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Alisema watoto wachanga wanachangia takribani nusu ya vifo vyote vya watoto walio chini ya miaka mitano, hivyo kuboresha huduma katika siku za mwanzo za maisha ni muhimu katika kupunguza vifo vya watoto kwa ujumla.
Alisema wizara itaendelea kuimarisha miongozo kuhusu usaidizi wa unyonyeshaji pamoja na huduma ya Kangaroo Mother Care, inayohusisha kumuweka mtoto ngozi kwa ngozi na mama yake.

Dk Magembe aliwataka wazazi na walezi kupuuza dhana potofu zinazowazuia wanawake kukamua maziwa ya mama, akisisitiza kuwa watoto ambao hawawezi kunyonya moja kwa moja wanaweza kupewa maziwa ya mama kwa njia salama zinazopendekezwa na wataalamu wa afya.
Hatua hizo zimekuja baada ya utafiti wa Low Birth Infant Feeding Exploration (LIFE) kubaini changamoto katika utoaji wa huduma kwa watoto wachanga katika nchi tatu za Tanzania, India na Malawi.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, daktari bingwa wa watoto, Profesa Karim Manji, alisema nchini Tanzania utafiti huo ulihusisha Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Amana na Hospitali ya Temeke.
Alisema utafiti ulibaini changamoto kuu nne ambazo ni kuchelewa kuanza kunyonyesha, ushauri duni kwa kina mama, udhaifu katika utunzaji wa kumbukumbu za kitabibu na ukosefu wa msaada wa kutosha kwa kina mama wanaohudumia watoto walio katika mazingira hatarishi.

Utafiti huo ulibaini kuwa ni asilimia tano pekee ya watoto wachanga waliohusishwa katika utafiti huo waliopatiwa maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.
Profesa Manji alisema ni asilimia 44 pekee ya kina mama waliopata aina fulani ya ushauri kuhusu unyonyeshaji, hali iliyowaacha wengi bila mwongozo wa kutosha kuhusu namna ya kuwalisha watoto ambao hawawezi kunyonya moja kwa moja.
Alisema kina mama wenye watoto waliozaliwa kabla ya wakati au wenye uzito mdogo mara nyingi huhitaji msaada wa vitendo katika kukamua maziwa ya mama, kuyahifadhi kwa usalama na kuwalisha watoto hao kwa njia inayofaa.

Utafiti pia ulibaini udhaifu katika kumbukumbu zinazoonyesha kiasi cha maziwa alichopata mtoto na mabadiliko ya uzito wa kila siku, hali inayofanya kuwa vigumu kwa wahudumu wa afya kufuatilia ukuaji na kubaini mapema changamoto za ulaji.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Apollinary Kamuhabwa, alisema tafiti zinapaswa kutafsiriwa katika maboresho ya huduma za afya kwa vitendo.
Alisema ushirikiano na taasisi za kimataifa, ikiwamo Chuo Kikuu cha Harvard na washirika wa utafiti kutoka Sweden, ni muhimu katika kuzalisha ushahidi unaoweza kusaidia kukabiliana na changamoto za afya nchini.

Alisema matokeo hayo yanatarajiwa kusaidia kuboresha namna watoto wachanga wanavyolishwa, kuongeza ujuzi wa wahudumu wa afya na kuimarisha msaada kwa mama wenye watoto wanaohitaji huduma maalumu.

Profesa Manji alisema kudhibiti joto la mwili, kuzuia maambukizi na kuhakikisha watoto wanapata lishe ya kutosha ni mambo muhimu katika kuongeza uwezekano wa kuishi na kukua vizuri kwa watoto walio katika mazingira hatarishi.



