SERIKALI ina mpango wa kuongeza misitu ya asili kwa kila halmashauri nchini kama njia ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira ambao baadae utasaidia kwenye biashara ya kaboni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Ashatu Kijaji amesema hayo mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo.
Dk. Kijaji ameeleza kuwa lengo ni halmashauri hizo kuingia kwenye biashara ya kaboni ambapo zoezi la kupandwa miti kwa pamoja kutawezesha faida kuonekana haraka kuliko kupandwa na mtu mmoja mmoja.
Waziri Kijaji ameongeza mpango huo utashirikisha zaidi wale ambao wana maeneo makubwa ya ardhi ambapo wanaweza kutumia ekari tano hadi kumi kwa ajili ya kupanda miti hiyo.
SOMA: Biashara ya kaboni motisha kuhifadhi mazingira
“Kufanikiwa kwa kupandwa miti hiyo kutasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo mengine yanasababisha ongezeko la joto pamoja na mvua ambazo hazina mpangilio mzuri,”amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dk. Batilda Burian amesema kumekuwepo changamoto ya wananchi kuchoma misitu hovyo hivyo Serikali na wadau inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuona namna ya kuzuia matukio hayo.
Ameongeza kuwa mkoa huo una zaidi ya hekta laki saba za misitu ambapo ndani yake kuna mashamba matatu ya miti.
Amesema lakini kumekuwa na changamoto ya wananchi kuvamia na kuingiza mifugo pamoja na kuchoma mkaa na mamlaka husika zinaendelea na udhibiti.
Amesisitiza kuwa katika mkoa huo wananchi pia wamekuwa wakijishughulisha na kilimo cha mikoko ambacho kinasaidia katika utunzaji wa mazingira ya bahari kwani wakati wa mmomonyoko wa udongo miti hiyo inasaidia kusitokee uharibifu kwenye maeneo ambayo mikoko ipo.