Serikali kuongeza usikivu wa TBC

WIZARA ya Habari, Mawasiliano wa Teknolojia ya Habari katika mwaka wa fedha 2023/24 imepanga kutekeleza mradi wa kuboresha upanuzi wa usikivu kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Hayo yamesemwa na Waziri Nape Nnauye leo, Mei 19, 2023 bungeni Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka 2023/2024.

Amesema katika utekelezaji wake wizara itaendelea kujenga na kufunga miundombinu ya utangazaji katika wilaya tisa kati ya wilaya 21 ambazo hazina usikivu au usikivu hafifu.

Nape amesema wataendelea na ujenzi wa makao makuu ya TBC Jijini Dodoma, ununuzi wa mitambo na vifaa vya utangazaji vya redio, Televisheni na mitandao ya kijamii kwa lengo la kuunganisha studio tano za Mikocheni, Zanzibar, Barabara ya Nyerere, Dodoma na Arusha pamoja na kununua gari moja ya kurushia matangazo ya Televisheni mbashara.

Kwa upande mwingine alisema wizara inapanga kutekeleza mradi wa kufunga mitambo mipya ya kisasa ya uchapishaji.

“Katika mradi huu tutakamilisha ujenzi wa majengo ya kiwanda cha uchapaji na kufunga mitambo ya kisasa ya uchapaji ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo magari kwa ajili ya kuongeza uzalishaji,” amesema waziri Nape

Habari Zifananazo

Back to top button