Serikali kuwalinda walimu kesi za wanafunzi
SERIKALI imeeleza nia ya kuwalinda walimu wanao simamia maadili kwa wanafunzi shuleni na vyuoni huku wakitakiwa kuendelea kuwasaidia wanafunzi katika malezi na maadili yenye misingi bora.
Imedaiwa walimu kutishiwa pale wanapofundisha maadili,wanapokwenda kutoa ushahidi kesi za kulawitiwa au ubakaji mahakamani na kupigiwa simu au kutumia jumbe za meseji waachane na masuala hayo.
Walimu waliyasema hayo jana kwenye mafunzo ya walimu wa malezi yaliyokuwa yakitolewana na Gerald Mwaitebele ambaye ni katibu msaidizi ofisi ya Rais Sekretariet ya Maadili Viongozi na Umma Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Tabora, Kigoma Simiyu na Shinyanga.
Mwaitebele alisema serikali ipo kazini hakuna mwalimu atakayewatisha kwani wameamua kuzunguka kila mkoa kuhamasisha uundwaji wa vilabu vya maadili mashuleni na vyuoni ili wanafunzi wajitambue na kuendelezwa maadili hayo pindi wawapo kazini na kwenye jamii inayowazunguka.
“Walimu tutawalinda wazazi wengine hawana tabia nzuri hilo linafahamika ukimuadhibu mtoto anakuja kakushikia kiuno shuleni pia mnapoitisha mikutano ya wazazi muweke mashairi na maigizo yenye ujumbe wa maadili ili wazazi waone wajifunze alisema Mwaitebele.
Kaimu ofisa elimu Mkoa wa Shinyanga ambaye ni mratibu wa maadili, Baraka Kasinyo akielezea suala la uzalendo alisema klabu hizo shuleni na vyuoni zitawafanya wanafunzi kuipenda nchi yao,kuitetea, uwajibikaji na kutii sheria,kudumisha demokrasia na kutunza rasilimali na wazazi watakao watishia walimu Serikali ipo na vyombo vyake vya sheria.
Akimwakilisha katibu tawala mkoa wa Shinyanga katibu tawala msaidizi Ibrahimu Makana alisema lengo la kuwepo klabu za maadili shuleni na vyuo vitawajenga wanafunzi katika misingi bora ya kuwa waadilifu na waaminifu tangu wakiwa shuleni.
Mwalimu Anael Yeunge kutoka shule ya msingi Town manispaa ya Shinyanga alisema masuala ya ulawiti kwa watoto yanatoka huko kwenye jamii na wazazi hawafuatilii na mwalimu kuja kugundua ni muda mrefu na anapokwenda kutoa ushahidi mahakamani wanakutana na vitisho.
Mwalimu wa shule ya msingi Kambarage Amos Nkungu alisema shule hiyo imezungukwa na vilabu vya pombe walevi wanapita na kutoa lugha chafu na watoto wamekuwa wakiiga hivyo Serikali ichukue hatua ya kupiga marufuku vilabu karibu na maeneo ya shule