Serikali, TLS, kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema serikali imeingia makubaliano na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuwa na kambi maalumu ya mawakili watakaotembelea magereza yote nchini kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa.
Dk Ndumbaro amesema hayo wakati akisikiliza matatizo na kuzungumza na wafungwa katika Gereza la Kiberege lililipo wilayani Kilombero mkoani Morogoro kupitia Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’.
Waziri Dk Ndumbaro ameagiza kuwa kambi hiyo ianzie mara moja katika Gereza la Kiberege, ambapo mawakili wa TLS watashiriki kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa wenye changamoto mbalimbali za kisheria.
“Niwape matumaini wafungwa katika magereza nchini lipo jopo la mawakili kutoka TLS watawafikia, kusikiliza na kushughulikia changamoto za rufaa mlizonazo,”
“Niwaombe muwe na subira wanasheria watakuja watawatengenezea rufaa zenu na kuzipeleka mahakamani, Rais Samia ameshaagiza kila mfungwa apate haki yake, kama umeonewa upate haki yako,”amesema Dk Ndumbaro.
Wakati wa zoezi hilo, Waziri Dk Ndumbaro ametoa msaada wa kisheria kwa wafungwa 15 na mahabusu wawili na amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuhakikisha haki inapatikana kwa wafungwa na mahabusu wote, hususan wale waliofungwa kwa makosa ya kusingiziwa.
Dk Ndumbaro amewahakikishia wafungwa kuwa kwamba serikali inaendelea kujizatiti kutoa msaada wa kisheria kwa wale wanaohitaji na kusisitiza wale waliofungwa kwa makosa halali watubu makosa yao na wakawe raia wema pindi watakapomaliza vifungo vyao.
Akijibu maombi ya baadhi ya wafungwa kutaka wahamishiwe kwenye magereza maeneo ya kwao ,Waziri amesisitiza kuwa kufungwa ni adhabu na kuwataka wasichague gereza.
“Mnakumbuka msemo usemao Mfungwa hachagui gereza hivyo popote unapopelekwa hakuna budi kukubali kwa maana Tanzania ni moja na wananchi wanahaki ya kuishi popote,”amesema Dk Ndumbaro.
Kwa upande wa makosa ya msamaha, Waziri Dk Ndumbaro amesema msamaha unaendana na matendo mazuri ya mfungwa anayotenda wakati wa kifungo chake gerezani.
“Yapo makosa makubwa ambayo hayana dhamana yakiwemo uhaini, mauaji, kujamihiana, ubakaji na uhujumu uchumi…haya makosa haya hayana dhamana, niwaombe tu Watanzania kujiepusha na makosa hayo ili wawe salama” amesema Waziri Dk Ndumbaro.
Dk Ndumbaro aliwaomba wafungwa hao kumwombea dua Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutokana na kuwafikiria na kuwaletea msaada wa kisheria ambao utawasaidia kutatua kero zao na kupata haki zao.


