Serikali, Uber wajadiliana kurejesha teksi mtandao
MAJADILIANO yanaendelea baina ya serikali, kampuni ya Uber na wadau wa huduma ya usafirishaji kabla ya kurejea huduma za teksi mtandao iliyokuwa imesimama.
Naibu Waziri Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya alibainisha hayo juzi bungeni na kuongeza kuwa kabla ya mwisho wa mwezi huu, serikali itakuwa imepata mwafaka wa suala hilo ili huduma hizo ziweze kurejea.
Alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mahonda, Abdullah Ali Mwinyi (CCM) aliyetaka kufahamu serikali imechukua hatua gani kutatua changamoto zinazoelezwa za ukiritimba zilizoifanya kampuni ya Uber kusitisha huduma zake nchini.
Kasekenya alisema serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilianza kudhibiti huduma za teksi mtandao Mei, 2020 kwa kutumia Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Na. 3 ya Mwaka 2019 pamoja na kanuni zake.
Alisema baada ya Latra kuanza kudhibiti eneo hilo kisheria, iliweka viwango vya tozo kwa huduma za teksi ili kupunguza migogoro kati ya madereva na wamiliki wa mifumo ya teksi ambao ni pamoja na Kampuni ya Uber.
Kutokana na hatua ya Latra kuweka tozo katika huduma za teksi mtandao, alisema kampuni ya Uber iliamua kusitisha kutoa baadhi ya huduma nchini Aprili, mwaka huu.
Alisema serikali inatambua huduma hiyo inachangia ajira kwa vijana na kuwa kupitia Latra inaendelea na mazungumzo na Uber kwa lengo la kuhakikisha inarejesha huduma za teksi mtandao.