KILIMANJARO: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema serikali ipo tayari kushirikiana na viongozi wa dini ili kuwawezesha kutimiza majukumu yao kwa Watanzania.
Dk Biteko amesema hayo leo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Mwanga, Kanisa Kuu lililopo mkoani Kilimanjaro wakati akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan mara baada ya ibada ya mazishi ya aliyekuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, Chediel Sendoro aliyefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Septemba 9, 2024 katika eneo la Kisangiro wilayani Mwanga.
“Rais yupo tayari kushirikiana na kanisa wakati wowote ili kanisa liweze kufanya kazi zote za kitume na sisi tuko tayari kuifanya Tanzania iwe bora na Watanzania waishi vizuri katika nchi yao,” amesema Dk. Biteko.
SOMA: Serikali inathamini mchango wa madhehebu ya dini
Ameongeza kuwa msingi wa dayosisi hiyo umejengwa kwa upendo na kuwa moja ya kazi kwa viongozi wa kanisa hilo ni kupata mtu atakayeendeleza kazi na maono ya Askofu Sendoro juu ya kanisa hilo.
Amefafanua kuwa kila binaadamu ataiaga dunia itakapofika wakati wake ispokuwa kila mmoja aliyehai amefanya nini na hivyo hawana budi kukumbuka mahubiri ya Askofu Sendoro na umoja alioujenga miongoni mwao.
“Natoa pole kwa familia, wazazi, mjane, watoto na wajukuu kwa kuwa Septemba 9, 2024 lilitokea jambo lisilo la kawaida na kuondokewa na Askofu Sendoro. Nakupa pole Askofu Mkuu wa Kanisa, maaskofu wote na Wanamwanga, tuyaenzi yote aliyokuwa akiyaishi, alijali sana maadili yetu naomba tena tuendelee kuliombea Taifa na nchi yetu,” amesisitiza Dk Biteko.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema kuwa Rais Samia alishatoa muongozo na uchunguzi ufanyike haraka iwezekanavyo juu hali ya siasa na vitendo vya uvunjifu wa amani nchini.
SOMA: Serikali yathamini michango taasisi za dini
“ Nataka niwaombe kama viongozi wa kiroho muendelee kushirikiana na Serikali kuwaombea Watanzania na kuifanya Tanzania kuwa mahali bora zaidi pakuishi,” amesema Dk. Biteko.