Serikali yathamini michango taasisi za dini

BUKOMBE, Geita: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema kuwa, Serikali inathamini na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na taasisi za kidini katika kusogeza huduma mbalimbali kwa wananchi mijini na vijijini.

Dk Biteko amesema hayo leo wakati alipotembelea Hospitali ya San Pio inayohudumia wagonjwa 2000 kwa mwaka wilayani Bukombe mkoani Geita akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella na viongozi wa Chama cha Mapinduzi.

Kwa kutambua mchango huo wa taasisi za kidini, Dk Biteko amesema kuwa, Serikali ipo tayari muda wote kushirikiana nao ili  kuendeleza yale wanayokusudia kuyafanya katika jamii.

Dk Biteko amepongeza uongozi na wafanyakazi wa Hospitali hiyo chini ya Mkurugenzi, Sista Teresa Goska, kwa kutoa huduma bora za kiafya kwa wananchi   na pia uamuzi wao wa kuanza kutoa huduma katika Sekta ya Elimu ambapo wameanza na darasa la awali.

Akiwa katika Hospitali hiyo ya San Pio, Dk Biteko aliwafariji wagonjwa mbalimbali waliolazwa na wanaosubiri huduma pamoja na kukagua majengo na miundombinu ya kutolea huduma hospitalini hapo.

Uongozi wa Hospitali hiyo umemshukuru Dk Biteko kwa kutembelea hospitali hiyo ikionesha kuwa, anatambua na kuthamini huduma inayotolewa kwenye hospitali ya San Pio ambayo ipo chini ya Jimbo Katoliki la Kahama.

Habari Zifananazo

Back to top button