Serikali yaagiza tathmini ujenzi kituo cha afya Mtwango

SERIKALI imetaka kufanyika tathmini ili kufahamu mahitaji kwa lengo la kuanza mchakato wa ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Mtwango iliyopo Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa.

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Deogratias Ndejembi ametoa agizo kwenda kwa mganga mkuu wa mkoa huo kutuma timu ya tathmini kisha aiwasilishe katika wizara hiyo ili serikali iangalie namna ya kupelekea fedha za ujenzi wa kituo hicho.

Ndejembi ametoa agizo hilo leo Juni 26, 2023 bungeni Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini, David Kihenzile aliyehoji ni lini serikali itajenga kituo cha afya katika kata ya Mtwango kwa kuwa kata hiyo haina kituo cha afya.

Advertisement

Akijibu swali hilo, Ndejembi amemhakikisha mbunge huyo kuwa serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

“Nimtoe mashaka Mheshimiwa Kihenzile serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele cha kujenga vituo vya afya kwenye maeneo yote ya kimkakati nchini ikiwemo kituo cha afya Mtwango.”amesema Ndejembi.