Serikali kuboresha ufaulu sayansi, hisabati na TEHAMA

ARUSHA: WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeeleza kuwa inachukua hatua madhubuti kuboresha ufaulu wa masomo ya Sayansi, Hisabati, na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini.

 

Wizara imesema kuwa walimu wa masomo hayo wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara kwa lengo la kuboresha ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.

 

Akizungumza jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum kwa walimu wa masomo ya Sayansi, Hisabati, na Tehama kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, Mratibu wa Kituo, Majaliwa Mkalawa, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha taifa linazalisha wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya Sayansi na Teknolojia.

Walimu wanaoshiriki mafunzo

“Kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini(SEQUIP), Wizara inaendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu ili kufundisha masomo hayo kwa kutumia mbinu bora na zenye kuvutia wanafunzi,” amesema Mkalawa.

SOMA: Smart Darasa kutatua changamoto masomo ya sayansi

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuboresha mbinu za ufundishaji kwa walimu ili kuwafanya wanafunzi kuyapenda masomo ya Sayansi, Hisabati, na Tehama, hivyo kusaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuchangia maendeleo ya kitaifa kwa kuzalisha wataalamu bora watakaosaidia kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.

 

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Taaluma wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Edith Chona, akizungumza kwa niaba ya Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha, amesema mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa walimu kuwafundisha wanafunzi kwa kutumia mbinu za kisasa na zinazolingana na mabadiliko ya teknolojia.

Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Edith Chona akifungua mafunzo hayo

“Mafunzo haya yatasaidia walimu kuwavutia wanafunzi kwenye masomo haya muhimu, jambo ambalo litachangia kuongeza ufaulu wao na kuhamasisha kupenda masomo ya Sayansi,” amesema Chona.

 

Dilioza Assenga, Mwalimu wa Somo la Baiolojia kutoka Shule ya Sekondari Ngarenaro, amesema anatarajia kujifunza mbinu zitakazosaidia kuboresha ufundishaji wake, hususan kwa wanafunzi wa kike, ili kuwahamasisha kushiriki zaidi katika masomo ya sayansi.

Wawezeshaji wa mafunzo

“Mbinu hizi mpya zitanisaidia kuwafanya wanafunzi, hasa wa kike, kuvutiwa na masomo ya sayansi, jambo ambalo litaimarisha ushiriki wao katika fani za kitaalamu baadaye,” amesema Assenga.

 

Zaidi ya Walimu 500 na Wathibiti Ubora wa shule kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wanashiriki mafunzo hayo maalum yanayofanyika katika Shule ya Sekondari Ilboru, jijini Arusha.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button