Serikali yaendelea kupambana changamoto ya umeme
LICHA ya upungufu wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme nchini, serikali imewatoa hofu watanzania ikisema mikakati mbalimbali inaendelea kufanywa katika kukabiliana na adha ya uzalishaji wa nishati hiyo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema upungufu huo unashughulikiwa kupitia vyanzo vingine ikiwemo kuongeza kiwango cha gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme na matengenezo ya mitambo iliyoharibika.
“Mtaona shida ya umeme imeanza kupungua na katika kipindi kisichozidi miezi sita tutakuwa tumepunguza au kuondoa kabisa tatizo la umeme nchini,” Dk Biteko alisema katika ziara yake aliyoifanya katika bwawa la Mtera kujionea hali halisi ya uzalishaji wa umeme.
Alisema mkakati umewekwa ili kuhakikisha pia maji yaliyopo katika mabwawa yote ya kuzalisha umeme nchini yanatumika kwa uangalifu mkubwa wakati mvua zikisubiriwa kunyesha katika kipindi cha miezi miwili ijayo na kujaza mabwawa hayo.
“Tumekuja kuona hali halisi na kuchukua tahadhari za mapema ambazo ziko ndani ya uwezo wetu na zile zinazoweza kutokea kesho tuweke mipango ya haraka itakayosaidia kupunguza shida ya umeme nchini,” alisema.
Amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji huku akizitaka idara zinazohusika na mazingira kuungana na kuja na mikakati ya ziada itakayookoa vyanzo hivyo.
“Vinginevyo uwekezaji huu na mitambo tunayonunua haitakuwa na maana kama tutaendelea kuharibu vyanzo vya maji,” alisema.
Pia amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kujenga utaratibu wa kuifanyia matengezo ya mara kwa mara mitambo yake ili kuepukana na adha ya kuharibika ambayo matokeo yake katika uzalishaji wa umeme ni mabaya.
Dk Biteko amesisitiza kwamba kazi ya Wizara ya Nishati ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme na akatoa wito kwa Tanesco kutilia mkazo ukarabati wa mitambo yake ili kuepuka matatizo yanayosababishwa na uharibifu huo.