SERIKALI imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri kutoidhinisha maombi ya kuhama yanayowasilishwa na watumishi wapya wanaopangiwa vituo vyao vya kazi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI) ametoa agizo hilo Bungeni, Dodoma leo huku akisema mtumishi anapaswa adumu katika kituo cha kazi alichopangiwa kwa angalau miaka mitatu mara baada ya kupata ajira.
“Mtumishi anapopangiwa kituo chake cha kazi hapaswi kuhama hasa katika kipindi cha probation [matazamio]. Nawaagiza wakurugenzi kutoidhinisha maombi hayo ya kuhama chini ya muda huo,” amesema Ndejembi.
Ndejembi ametoa agizo hilo wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu baada ya wabunge kutoka mkoa wa Lindi Salma Kikwete (Mchinga) na Zuber Kuchauka (Liwale) kuitaka Serikali kueleza mkakati wa kudhibiti watumishi wa afya wanaopangiwa kwenye halmashauri lakini huondoka na kuacha maeneo hayo kubaki kuwa na upungufu.
Hata hivyo, Naibu Waziri amesisitiza watakaopata ajira zilizotangazwa hivi karibuni watadhibitiwa kupitia mkakati huo pia.
Katika swali lake la msingi, Mbunge wa Viti Maalum, Minza Mjika alitaka kufahamu lini Serikali itaongeza watumishi wa afya katika hospitali ya wilaya ya Meatu.
Akihibu swali hilo, Ndejembi amesema Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya.
Katika mwaka wa fedha 2021/22, jumla ya watumishi 7, 736 wa afya waliajiriwa huku Halmashauri ya wilaya ya Meatu ilipangiwa watumishi 104.
“Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2022/23, Serikali itaajiri watumishi wa Kada ya Afya 8,070. Aidha, baada ya taratibu za ajira kukamilika watumishi hao watapangwa kwenye Halmashauri zote nchini ikiwemo
Halmashauri ya Meatu,” alihitimisha jibu lake.