Serikali yaja na mpango ajira kwa madaktari

DAR ES SALAAM  – NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kupanua wigo wa ajira hususani katika sekta ya afya kutokana na ongezeko la wahitimu.

Katambi ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kufungua Kongamano la Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) ambalo wataalamu zaidi ya 300 wamekutana kujadiliana mambo mbalimbali.

Alisema katika kukabiliana na ongezeko la wahitimu kila mwaka hususani wa sekta ya afya, serikali imeingia makubaliano na nchi kadhaa kwa ajili ya kutanua wigo wa ajira kwa wasomi nchini. Alisema mpango huo umeanza kutekelezwa kwa kuanza na kada ya wauguzi 500 kisha watafuatia madaktari.

“Lakini kuna suala la kukidhi vigezo, tuhakikishe tunalifanikisha kwa kuendelea kujitafutia ujuzi wa kutosha,” alisema. Aliwashauri madaktari kutumia fursa za nchi nyingine zaidi ya nane zinazoizunguka Tanzania ambazo bado zinahitaji madaktari bingwa kwenda kujipatia ajira wakati huu ambao serikali inaendelea kukabiliana na tatizo la ajira kwa madaktari 5,000 waliopo mitaani.

Awali, Rais wa MAT anayemaliza muda wake, Dk Deus Ndilanha alisema changamoto iliyopo ni ajira na kwamba zaidi ya madaktari 5,000 wako mitaani bila ajira. “Hata waliopo kwenye ajira baadhi yao wamekwama kupanda vyeo vya kiutumishi kwa muda mrefu sasa, tuombe serikali kuliangalia hili maana kada hii ni nyeti na inatakiwa kuangaliwa kwa unyeti wake,” alisema.

Aidha, katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi na Dk Merida Makia ambaye ni Mshauri mwelekekezi wa fani hiyo, walitunikiwa tuzo ya utumishi uliotukuka.

Habari Zifananazo

Back to top button