KATAVI: AGIZO la Rais Samia Suluhu Hassan la kumtaka Waziri mwenye dhamana ya Ardhi Jerry Silaa kumaliza mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa Mtaa wa Rungwa Kata ya Kazima Mpanda Katavi na Chuo cha Kilimo Katavi (KUA) limetekelezwa baada ya Waziri wa Ardhi Jerry Silaa kukabidhi hatimilki za ardhi kwa wananchi hao.
Akiongea katika hafla fupi ya kukabidhi hatimilki za ardhi kwa wananchi hao Waziri Jerry Silaa amesema amefanikiwa kumaliza mgogoro huo kufuatia taarifa ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Daniel Chongolo kwa Rais Samia alipohitimisha ziara yake mkoani Katavi, hivyo Rais kutoa agizo la kukamaliza mgogoro huo.
Waziri Silaa amebainisha kuwa Rais Samia alimuagiza kumaliza mgogoro huo baada ya kuwa amepata taarifa kutoka kwa viongozi wa mkoa na Chama na kuongeza kuwa alimtaka kuhakikisha mwaka mpya ujao unaanza bila ya kuwa na mgogoro wowote.
‘’Nilikuja hapa Oktoba 7, mwaka huu na kutoa maagizo kwa Wizara ya Ardhi kuhakikisha inatekeleza maagizo ya Rais,Samia Suluhu Hassan kwamba mgogoro huu ufike mwisho na niwambie tangu nipate uteuzi na kupewa maelekezo ya nini kifanyike sijawai kukutana na mgogoro wa ardhi ambao hautatuliki.’’Amesema Silaa
Katika hatua nyingine Waziri Silaa ameagiza Uongozi wa Mkoa wa Katavi pamoja na wananchi wa Kitongoji cha Rungwa kuhakikisha wanalinda maeneo 13 ya wazi,hospitali, masoko,makaburi na maeneo ya shule za awali pamoja na shule za msingi na sekondari.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi Iddi Kimanta amebainisha kuwa kuna viongozi wengi mkoani Katavi ambao kwa kipindi kirefu waliangaika na mgogoro huu bila mafanikio lakini jana Waziri mwenye dhamana ya ardhi alifanikiwa kumaliza mgogoro huo.
Kufuatilia hali hiyo Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Katavi alimtaja Waziri mwenye dhamana ya Ardhi Jerry Silaa kuwa anaingia kwenye historia kwa kufanikiwa kumaliza mgogoro huo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusufu amehaidi kuwa, kwa kuwa mgogoro huu umekwisha basi hawatakubali kuona unazalisha mgogoro mwingine kwenye neo hili maarufu hilo.