Serikali yaongeza kasi elimu, afya na ajira

SERIKALI imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha sekta za elimu, afya na ajira kwa lengo la kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Akiwasilisha Mapitio na Mwelekeo wa kazi za Serikali pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2026/2027, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amesema katika sekta ya elimu Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Elimu Bila Ada kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari ya juu.
“Serikali imeendelea kutekeleza Mpango wa Elimu Bila Ada kwa kugharimia elimu ya awali hadi elimu ya sekondari ya juu. Hadi Februari, 2026 shilingi bilioni 383.22 kati ya shilingi bilioni 510.96 sawa na asilimia 75 zimetolewa kwa shule za msingi 18,119 na shule za sekondari 5,179,” alisema.
Amesema sambamba na hilo, Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (VETA) katika wilaya mbalimbali ili kusogeza huduma karibu na wananchi. “Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa vyuo vya VETA 64 vya wilaya ambao umefikia wastani wa asilimia 67,” alisema.

Kuhusu elimu ya juu, Dk. Mwigulu amesema Serikali imeendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi pamoja na ufadhili kupitia programu ya Samia Scholarship. “Jumla ya shilingi bilioni 899.21 zimetolewa katika mwaka 2024/2025,” akibainisha kuwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu wameendelea kufadhiliwa kusoma masomo ya sayansi ndani na nje ya nchi.
Katika sekta ya afya, Dk. Nchemba amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma kuanzia ngazi ya zahanati hadi huduma za ubingwa na ubingwa bobezi. “Ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bingwa na bobezi, Serikali inatekeleza mikakati mahsusi ya kuongeza madaktari bingwa na bingwa bobezi,” alisema.
Hatahivyo. Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba ameongezea kuwa Serikali imeimarisha mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kuongeza vyanzo vya fedha vya ndani.“Hadi Februari, 2026 Serikali imekusanya shilingi bilioni 26.8 kupitia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI,” alisema.
Akizungumzia ustawi wa jamii, Dk. Mwigulu amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu kwa kutoa ruzuku, vifaa saidizi na huduma za afya. “Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu imetoa ruzuku ya shilingi milioni 238.92 kwa vyama 13,” alisema.
Katika sekta ya ajira amesema hadi Februari 2026 jumla ya ajira 625,273 zimezalishwa, huku Watanzania pia wakipata fursa za ajira nje ya nchi.“Serikali imewezesha upatikanaji wa ajira 6,367 kwa Watanzania katika nchi za Saudia, Qatar, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu,” alisema.
Kwa upande wa utumishi wa umma, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa kupandisha vyeo, kuajiri na kulipa madai mbalimbali. “Serikali imepandisha vyeo na madaraja watumishi 662,707 na kuajiri watumishi wapya 155,008,” alisema.

Katika kuimarisha usalama, Serikali imeendelea kuviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. “Vifaa na mitambo ya kuzima moto yenye thamani ya dola za Marekani milioni 100 imenunuliwa na kusambazwa mikoa yote nchini,” alisema. SOMA: Ayoub ahimiza ufanisi huduma zimamoto
Kwa mwaka 2026/2027, Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika elimu, afya, ajira na usalama ili kuchochea uchumi wa viwanda na ustawi wa wananchi. “Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya na kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia,” alisema. Aidha, amewataka wazazi na walezi kushirikiana katika malezi bora ya watoto ili kujenga taifa lenye maadili, uzalendo na lenye nguvu kazi yenye tija.




I earned $17,932 last month by working online for just 2 hours a day. This job is simple, flexible, and beginner-friendly,S1 making it accessible to everyone. It has helped me manage my finances effortlessly while focusing on my education as a full-time student.
You can click on this the website and begin
right away…. www.work27.online