Serikali yaonya upotoshaji utekaji watoto

DAR ES SALAAM; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameonya kuhusu kuibuka  watu na baadhi ya vyombo vya habari kusambaza taarifa za uwongo kwenye jamii kuhusu kupotea au kutekwa watoto, hivyo kuzusha taharuki kwa jamii.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Waziri Masauni amesema  watu hao wamekuwa wakitumia taarifa za zamani na kuleta taharuki kwa jamii.

“Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,kupitia Jeshi la Polisi, inafuatilia kwa karibu na itawachukulia hatua wote watakaobainika kujihusisha na tabia hiyo.

Advertisement

Soma pia: Serikali yatoa tamko matukio utekaji

“Ikumbukwe kuwa kusambaza taarifa za uongo na zisizo na uhakika ni kosa kisheria na ikibainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yako.

“Ili kudhibiti matukio yote hayo na kuepusha taharuki iliyojitokeza nchini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi na kwa kushirikiana na wizara nyingine na vyombo vingine vya dola imeweka mkakati madhubuti,”amesema Mhandisi Masauni.

Amesema mkakati huo unahusisha mambo mablimbali ikiwemo kuongeza elimu kwa umma kuhusu utoaji wa malezi bora na ulinzi kwa watoto.

“Kwenye hili tutaongeza nguvu zaidi kwa Polisi Kata nchini nzima na pia kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Elimu kufikia na kutoa elimu kwa wananchi kwa urahisi.”amesema Mhandisi Masauni na kuongeza:

“Tutaimarishadoria za mara kwa marana kutoa kipaumbele kwenye taarifa wezeshi kutoka kwa wananchi wema. Hii ni pamoja na kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa haraka pale matukio kama hayo yanaporipotiwa Jesho la Polisi.”

Amesema serikali itaharakisha uchunguzi wa kesi zote za watuhumiwa ambao watabainika kujihusisha na masuala ya uhalifu wa watoto, ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa haraka.