Serikali yatoa tamko matukio utekaji

Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.

DAR ES SALAAM; SERIKALI imesema Tanzania iko salama dhidi ya vitendo vya utekaji na
inachukua hatua kuhakikisha watu wote waliohusika na utekaji nyara watu wanachukuliwa hatua za kisheria.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema vyombo vyao
vya ulinzi vina uwezo wa kuwapata watuhumiwa wa vitendo hivyo na kuwachukulia hatua za kisheria.

Alisema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza katika hafla ya kuzindua
kitabu cha Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar bin Zuberi cha Mmomonyoko wa maadili, nani alaumiwe?

Advertisement

Masauni alisema matukio ya utekaji ambayo yamekuwa yakitajwa mara kwa mara wanasiasa wamekuwa wakiyahusisha na serikali na vyombo vya usalama vilivyopewa dhamana ya kulinda watu.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo tangu kuanza kwa mwaka huu matukio ya utekaji yanayofanywa na
watu wasiojulikana hayazidi manane.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/zitto-ataka-uchunguzi-huru-vitendo-vya-utekaji/

Ametaja matukio hayo la kwanza ni la Juni 24, mwaka huu ambalo limetokea Dar es Salaam likihusisha mtuhumiwa ambaye alimteka nyarA msichana na kumbaka.

Alisema tukio lingine lilitokea Katavi ambalo linahusu watuhumiwa wanne na kesi yao iko mahakamani.
“Tukio la Juni 17, mwaka huu la mtoto Asimwe lililotokea Muleba, tunasikitika hatukuweza kumpata kabla
hajafariki lakini watuhumiwa wote tisa wamekamatwa na kesi inaendelea mahakamani,” alisema Masauni.

Pia alitaja tukio la Juni 24 mkoani Geita ambalo mtoto alitekwa na mtuhumiwa
alipigia simu wazazi wake ili wampatie fedha, mtuhumiwa na mtoto wote walipatikana.

Masauni alisema tukio lingine la utekaji kujipatia kipato lilitokea Februari 12, mwaka huu
Handeni mkoani Tanga.

“Tukio lingine lilitokea Machi 15 mkoani Mbeya na Mei 29, mwaka huu Geita na tunaendelea na uchunguzi kuwapata watuhumiwa wote,” alisema Masauni.

Alisema uchunguzi unaendelea kuhusu tukio la utekwaji mkazi wa Mbezi wilayani Ubungo, Edgar Mwakabela (27) maarufu Sativa anayedaiwa kutoweka Juni 23, mwaka huu na kupatikana mkoani Katavi akiwa na majeraha.

“Hii ndio hali halisi ambayo tunaambiwa serikali na polisi tunahusika na kwamba Tanzania hakukaliki. Lakini sisi tunachukua hatua na wote wanaohusika watakamatwa na kufikishwa katika vyombo
vya sheria,” alisema Masauni.