Serikali yaonya wanaotafuna fedha za umma

DODOMA- SERIKALI imeonya maofi sa masuuli na wengine wanaotumia vibaya fedha za umma. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ametoa onyo hilo bungeni Dodoma juzi wakati akiwasilisha mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Dk Mwigulu alisema serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti, Sura 439; Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348; Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290; Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410; na Sheria ya Matumizi ya Fedha za Umma ya Mwaka 2024. Alisema serikali itaendelea kuhakikisha sheria hizo zinasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kujibu hoja zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na hoja za wakaguzi wa ndani.

“Na endapo itabainika Ofisa Masuuli wa fungu husika ameshindwa kutekeleza matakwa ya sheria hizo, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa,” alionya Dk Mwigulu.

AGIZO

Aliagiza maofisa masuuli kuzingatia Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Namba 2 wa Mwaka 2021 kuhusu utaratibu wa kutumia magari, aina na stahili za magari kwa viongozi katika utumishi wa umma kwa lengo la kupunguza matumizi.

Alitaja hatua nyingine za kupunguza matumizi zitakazochukuliwa ni kupunguza safari za ndani na nje na kupunguza ukubwa wa uwakilishi kwenye mikutano ya ndani na nje ya nchi. “Vilevile, niendelee kuwasisitiza maofisa masuuli wote kuendelea kufanya vikao/mikutano kwa njia ya mtandao na kupunguza matumizi ya karatasi,” alisema. Aliongeza:

“Aidha, niwasihi viongozi wenzangu kuona umuhimu wa kusimamia matumizi ya fedha za umma ili kuleta maendeleo kwa wananchi. Na niwaonye wale wachache wanaotumia vibaya fedha za umma waache mara moja! Na wale watakaobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao”.

Alibainisha kuwa hatua za udhibiti matumizi ya fedha za umma zitaokoa fedha zitakazoelekezwa kwenye miradi itakayosaidia jamii kama vile ujenzi wa barabara, vituo vya afya, miundombinu ya maji na shule.

Alihimiza taasisi zote za serikali zizingatie taratibu za ununuzi wa umma na kuhakikisha ununuzi wote unaidhinishwa na bodi za zabuni ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa ununuzi na hivyo, kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

SOMA: Wasomi, wanasiasa wakoshwa bajeti 2024/25

“Nawaelekeza maofisa masuuli kuendelea kutumia mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kandarasi pamoja na kuzingatia bei ya soko wakati wa ununuzi,” alisema Dk Mwigulu.

Alisema serikali itaendelea kutekeleza mkakati wa kugharamia miradi ya maendeleo kwa kutumia vyanzo mbadala ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa bajeti ya serikali kuu.

Dk Mwigulu alisema mfano halisi wa utekelezaji wa mkakati huo ni kufanikiwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa) kutoa hatifungani ya kijani yenye thamani ya Sh bilioni 53.1.

Habari Zifananazo

Back to top button