Wasomi, wanasiasa wakoshwa bajeti 2024/25

DAR ES SALAAM – WASOMI, wanasiasa na wachumi wamepongeza bajeti ya serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 huku wakiishauri serikali kuendelea kutafuta vyanzo vingine vya mapato.

Juzi, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 bungeni.

Katika bajeti hiyo serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh trilioni 49.35. Akizungumza na gazeti hili jana Mhadhiri na Mkuu wa Idara Msaidizi ya Biashara na Rasilimaliwatu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya (CUoM) Samson Mwigamba, alipongeza bajeti lakini anadhani wizara bado haijabuni vyanzo vipya vya mapato.

“Lakini pia kuanza kutoza ushuru kwenye michezo ya kubahatisha na sehemu iende kwenye afya ni jambo zuri,” alisema. Kuhusu kikokotoo kuongezwa, Mwigamba alisema angefurahi serikali ingekuwa inapandisha mwaka hadi mwaka.

SOMA: Bajeti ya tril 49/- kuleta nafuu

“Pia napongeza uamuzi wa serikali kutoza gharama kwa fedha ya Tanzania badala ya kutumia Dola za Marekani, hii izingatiwe kama mtalii anakwenda mbugani aambiwe bei kwa fedha ya Tanzania,” alisema.

Mhadhiri wa Biashara, Ujasiriamali Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (SAUT) na mchambuzi wa masuala ya biashara na uchumi, Sylivester Jotta alisema bajeti hiyo imeangalia na kugusa maisha ya watu hasa wastaafu.

“Kwa sasa kuna ahueni kwa wastaafu asilimia imepanda hadi 40 kama ambavyo tunafahamu baada ya kustaafu wengi huwa wanategemea kiinua mgongo, na isivyo bahati ni wachache ambao huishi muda mrefu na kufaidi mafao yao, nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio cha wastaafu,” alisema Dk Jotta.

Kwa upande wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imesema bajeti imebeba unafuu wa maisha kwa kuboresha huduma mbalimbali.

Habari Zifananazo

Back to top button