Serikali yapewa mbinu kuteka soko DRC

WACHAMBUZI wa masuala ya diplomasia na uchumi wameishauri serikali iweke mikakati ya kunufaika na soko la dhahabu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ili kuongeza kasi ya kukuza uchumi, kuongeza fursa za biashara na ajira.

Wamesema DRC ina zaidi ya watu milioni 80 hivyo ni soko ambalo kupitia ujenzi wa miundombinu ya barabara na Reli ya Kisasa (SGR), itawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kununua dhahabu na kupeleka bidhaa nyingine za vyakula.

Juzi, Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Felix Tshisekedi wa DRC walishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), posta na mawasiliano.

Nchi hizo zimekubaliana kushirikiana kuendeleza sekta ya mawasiliano kwa kuwa ni sekta pekee inayozalisha rasilimali na ajira kwa vijana kwa kiasi kikubwa.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Dk Lawi Mamboleo alilieleza HabariLEO jana kuwa hati hiyo ya makubaliano itarahisisha mawasiliano na kukuza biashara.

“DRC ina rasilimali nyingi za madini ya aina mbalimbali, hivyo ujenzi wa miundombinu hiyo itawezesha Bandari ya Dar es Salaam kupata mzigo mkubwa zaidi ambao utawezesha kuongezeka kwa mapato bandarini. Nchi ya Congo inaongoza kwa kusafirisha shehena kubwa ya mzigo kupitia bandari hizi,” alisema Dk Mamboleo.

Aliongeza kuwa ni wakati kujenga miundombinu hiyo haraka kwa sababu kuna ushindani kwa nchi jirani ambazo zina bahari ikiwamo Kenya.

Dk Mamboleo alieleza kuwa Tehama itarahisisha biashara kwa kuongeza ufanisi na kupunguza urasimu.

“Tuimarishe mkongo wetu ili tunapokwenda kuteka soko la Congo tuwe imara kwenye mawasiliano kwa kuwa itapunguza gharama za usafiri, muda na kupunguza upotevu wa mapato hivyo ni vema mifumo yetu ya mawasiliano iwe imara kurahisisha biashara,” alisisitiza.

Mchambuzi wa masuala ya diplomasia ya uchumi, Abbas Mwalimu alisema serikali ina vyombo vinavyosimamia mawasiliano ikiwamo Mkongo wa Taifa, na DRC ni nchi ya kimkakati kwa sababu ina watu zaidi ya milioni 80 hivyo ni soko kubwa la biashara kwa Tanzania.

Alisema kutokana na mazingira yao, kuna fursa nyingi za kilimo kwa kuuza mazao ya chakula na biashara, kununua dhahabu inayozalishwa humo inayouzwa na kuuza kwa bei kubwa.

“DRC inatumia Bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 50 kusafirisha mizigo mbalimbali na kwa kuwa imeingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulinzi na usalama wa nchi hiyo unaimarika hivyo uchumi wa Tanzania utakua,” alisema Mwalimu.

Alisema anaamini ujenzi wa barabara ya Ushoroba wa Kati utasaidia kuongeza mwingiliano wa watu na mizigo endapo wataondoa vikwazo ikiwamo matumizi ya viza.

Alisema ni lazima nchi iweke mikakati ya kuliteka soko la DRC kwa kuhakikisha inafungua mikoa ya Katavi na Kigoma ili kuvutia wawekezaji.

“Rais Samia amepambana kuhakikisha inaufungua Mkoa wa Kigoma kwa kuondoa changamoto ya umeme, wanahitaji kuwekeza zaidi katika kujenga miundombinu wezeshi ya ndani ikiwemo kuingia mikataba ya kujenga barabara kwenda Kalema kwa gharama zetu ili inufaishe na kukuza uchumi wetu,” alisema Mwalimu.

Alisema serikali ni muhimu iweke mikakati kwa nchi inazoungamana nazo kwa kujenga viwanda vya bidhaa ili kuongeza ajira kwa wananchi, kuongeza thamani ya fedha, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na mizigo, pia kuhamasisha wafanyabiashara kuwekeza kwenye mikoa ya pembezoni.

Mchambuzi wa siasa na uchumi, Profesa Humphrey Moshi alisema makubaliano yaliyoingiwa juzi ni hatua kubwa kwani inalenga kukuza uchumi wa nchi zote.

Alisema soko la biashara kwa EAC limeongezeka kwa sababu DRC ina rasilimali nyingi za madini na kwamba ujenzi wa barabara utapanua mawasiliano kati ya Watanzania na DRC, kuongeza ajira na kukuza uchumi.

“Nchi ya DRC haina mawasiliano katika maeneo mengi, hivyo barabara hiyo pia itasaidia kupunguza migogoro katika mipaka na kuleta amani ili biashara iweze kufanyika kwa mafanikio,” alisema Profesa Moshi.

Aliongeza: “Tutatumia bandari zetu kupeleka vifaa mbalimbali Congo hivyo tutapata mapato, tutakuza uchumi na kukuza sekta za mawasiliano.”

Pia alisema kutakuwa na fursa nyingi za kukuza ajira na vipato vya wananchi kupitia biashara mbalimbali.

Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Lucy Mbogoro alisema manufaa ya mkataba huo kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya mawasiliano na posta, hivyo wataendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuvutia zaidi wawekezaji kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa kasi.

Pia wataendelea kuelimisha umma kubadili fikra ili kutumia Tehama kupata maendeleo, na kuwahimiza wananchi kutumia vifaa vyao vya mawasiliano kusaka fursa za kibiashara kujiingizia kipato ikiwamo kuuza mazao.

Rais Tshisekedi aliondoka Dar es Salaam jana baada ya kumaliza ziara ya kiserikali ya siku mbili nchini.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button