DODOMA: Bunge limeipa serikali miezi minne, hadi mwezi wa sita mwaka huu 2024 kuhakikisha nchi inapata umeme wa uhakika.
Uamuzi huo umetolewa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson baada ya Naibu waziri wa Nishati Judith Kapinga kusema mgao utapungua kwa mwezi huu wa pili kwa kiasi kikubwa na mwezi wa tatu mgao kuisha kabisa.
Spika amesema kwa kuwa muda wa awali ulikuwa mwezi wa sita lakini wakapunguza na kusema mgao utaisha mwezi wa 3, basi Bunge limeiongezea muda serikali na hivyo mpaka mwezi wa sita wawe wamemaliza tatizo la mgao nchini.
“”Wacha tuipe serikali muda, kwa maana ipi wao walijipanga mwezi wa sita (shida ya umeme kuisha) wakarejesha nyuma mwezi wa pili, tunawapongeza sana na mmerejesha mpaka mwezi wa tatu kwa hizo mashine zote kukamilika, Bunge linawapa mpaka mwezi wa sita ili bunge linapokuwa hapa mgao uwe umeisha, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri,”amesema Tulia
Awali akizungumza Kapinga amesema “mradi wa umeme wa Julius Nyerere ni moja ya mradi unaotekelezeka kwa weledi mkubwa sana, sote tunajua mwezi wa sita mwaka huu ndiyo tulitegemea kuwasha mtambio namba tisa kwa mara ya kwanza lakini kwa jitihada za serikali na wakandarasi tuliweza kusogeza ratiba za kuwasha mtambo huu hadi mwezi wa pili;……. “jana tumefanikiwa kufanya majaribio kwa ukamilifu kwenye mtambo namba tisa na tumeutembeza kwenye uwezo wake wa mwisho wa megawati 235,”
“Tuliahidi mwezi huu tuna ratiba ya kuzindua mtambo huu na ratiba hii iko palepale, tunawashukuru sana Watanzania kwa kuendelea kutuvumilia, matumizi ya umeme yanategemeana tukizalisha mwezi huu mgao utakuwa umepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu tunazalisha megawati 235 na mwezi wa tatu tutazalisha megawati 235 hivyo zitakuwa megawati 470 uhakika ni kwamba kufikia mwezi wa tatu mgao wa umeme utaisha nchini,” amesema Kapinga.
Kufuatia kauli hiyo, Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Tulia Ackson, amesema kuwa Bunge limewapa Tanesco muda kufikia mwezi wa sita mgao wa umeme uwe umeisha.