Serikali yasifu watumishi ujenzi uchumi

SERIKALI imesema utumishi wa umma ni nguzo muhimu katika uendeshaji na uendelezaji wa nchi na umeendelea kutoa mchango ulioiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kipato cha kati cha kiwango cha chini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema hayo bungeni Dodoma jana wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Simbachawene alisema serikali ina matarajio makubwa kuwa mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo utaendelea kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati wa kiwango cha juu.

Alisema maendeleo hayo yanatarajiwa kuongezeka kwa kuimarisha uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu kama inavyobainishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano Awamu ya Tatu.

Simbachawene alisema Mpango na Bajeti kwa mwaka 2023/2024 umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025.

Wabunge walielezwa kuwa bajeti hiyo pia imezingatia Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/2026) wenye dhima ya Tanzania kuwa na uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu na hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia Bunge Aprili 22, 2021.

Simbachawene alisema bajeti ya mafungu yote katika wizara hiyo yamelenga kuwa na utumishi wa umma unaotoa huduma bora kwa haraka na staha ukizingatia Katiba, sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika kujenga imani zaidi kwa wananchi na kuendana na kauli ya Rais Samia aliyoitoa katika hotuba hiyo ya bungeni.

Alieleza kuwa jitihada zaidi zitawekwa kujenga uwezo na mifumo ya kimenejimenti na utoaji huduma yakiwamo matumizi sahihi na salama ya fursa zinazopatikana katika utoaji huduma kwa tehama ndani ya serikali.

“Kupitisha bajeti hii ni njia ya kuimarisha na kuchangia kukuzwa kwa maadili kwa viongozi wote na watumishi wa umma kwenye nchi hivyo kupata tija ya rasilimaliwatu na rasilimalifedha kwa kuwa na matumizi yenye tija ya rasilimali hizo kwa wakati wote,” alisema Simbachawene.

Alisema katika bajeti hiyo serikali itayapa kipaumbele maeneo ya usimamizi wa rasilimaliwatu na rasilimalifedha.

“Vilevile, bajeti itaiwezesha serikali kupandisha vyeo watumishi; ubadilishwaji wa kada au muundo wa utumishi; kulipa malimbikizo ya mishahara ya watumishi na kutoa ajira mpya,” alifafanua Simbachawene.

Alisema serikali inafanya maboresho ya kisekta na mtambuka na wajibu wa Ofisi ya Rais itakuwa ni kuhakikisha maboresho yanayofanywa yanaleta tija katika utumishi wa umma na kuchochea maendeleo.

“Katika kuimarisha misingi ya utawala bora ya ushirikishwaji, uwazi na uwajibikaji, Ofisi ya Rais itahakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu maamuzi ya serikali na kuweka imara mifumo ya mrejesho wa utoaji huduma,” alisema Simbachawene.

Alisema mipango na bajeti hiyo imezingatia vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita kwenye eneo la kuimarisha utendaji kazi wa utumishi wa umma na kuiwezesha nchi iondokane na matumizi mabaya ya rasilimali fedha, ukiukwaji wa maadili ya uongozi na kupunguza urasimu katika utoaji huduma.

Habari Zifananazo

Back to top button