Serikali yataka bunifu za kitaifa kufika sokoni

DAR ES SALAAM: SERIKALI imevitaka vyuo vikuu na taasisi za utafiti nchini kuhakikisha bunifu zinazozalishwa kupitia tafiti za kisayansi zinageuzwa kuwa bidhaa na teknolojia zinazoweza kuzalishwa na kuuzwa sokoni, badala ya kubaki katika hatua ya maonesho.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, aliyesema sayansi, teknolojia na ubunifu ni nguzo muhimu katika kukuza viwanda, kuongeza ushindani wa uchumi na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Profesa Mkenda alisema Tanzania inapaswa kuimarisha uwezo wake wa kiteknolojia ili kupunguza utegemezi wa wataalamu na teknolojia kutoka nje, hususan katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Alisema matokeo ya tafiti yanapaswa kuendelezwa hadi kufikia hatua ya uzalishaji wa kibiashara ili yaweze kutoa mchango wa moja kwa moja katika uchumi na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
“Hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kufikia maendeleo endelevu bila kuhakikisha kuwa maendeleo yake yanaongozwa na sayansi, teknolojia na ubunifu,” alisema.
Miongoni mwa bunifu alizozitaja ni Mkanda Salama, kifaa tiba kilichobuniwa kudhibiti kutokwa na damu nyingi kwa wanawake baada ya kujifungua, ambacho tayari kimeonesha kuvutia mataifa ya Rwanda na Ethiopia.
Bunifu nyingine ni chanjo iliyotengenezwa nchini kwa ajili ya samaki wanaofugwa, pamoja na teknolojia ya kuzalisha gesi za haidrojeni na oksijeni kutoka kwenye maji, ambayo inaendelea kufanyiwa tathmini ili kubaini usalama wake na uwezekano wa kutumika kibiashara.
Pia alitaja ubunifu wa saruji uliofanywa na mwanafunzi wa shahada ya uzamivu kutoka Ethiopia katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela, unaotumia pozolana na chokaa kuzalisha saruji imara zaidi, yenye gharama nafuu na inayohitaji nishati kidogo wakati wa uzalishaji.
Alisema majadiliano yanaendelea na wazalishaji wa saruji ili kuweka mazingira ya kuanza uzalishaji wa kibiashara baada ya kukamilisha taratibu za kulinda haki miliki za ubunifu huo.
“Hatutaki bunifu zinazofanywa kwa ajili ya kuoneshwa kwenye maonesho pekee. Tunataka bunifu zinazofika sokoni na kuanza kuzalisha bidhaa,” alisisitiza.
Katika kuimarisha uzalishaji wa bidhaa nchini, Profesa Mkenda alisema Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeelekezwa kubaini aina za vipuri vya pikipiki vinavyoagizwa kwa wingi kutoka nje ambavyo vinaweza kuzalishwa nchini, kwa kuanzia na vile visivyohitaji teknolojia ya juu kabla ya kuelekea kwenye uzalishaji wa vipuri changamani zaidi.
Alisema DIT tayari inazalisha baadhi ya vipuri vya mifumo ya breki za magari, ikiwemo malori aina ya Fuso, na imepewa muda wa kuanzisha kampuni itakayoshughulikia uzalishaji na uuzaji wa bidhaa hizo.
Kuhusu tafiti za afya, Profesa Mkenda alisema Serikali inataka vyuo vikuu kufanya tafiti za kisayansi zitakazobaini ufanisi, kiwango sahihi cha matumizi na madhara yanayoweza kusababishwa na mimea tiba kabla ya kupendekeza matumizi yake katika matibabu.
“Tunataka sayansi iongoze matibabu badala ya kutegemea makisio,” alisema, akibainisha kuwa Tanzania inahitaji kuimarisha uwezo wa kufanya majaribio ya awali na majaribio ya kitabibu ili kuthibitisha usalama na ufanisi wa tiba mbalimbali.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha tafiti katika sekta za kilimo, uvuvi na mifugo ili kuhakikisha bunifu za kisayansi zinatoa majibu ya changamoto zinazozikabili sekta hizo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Aidha, aliwataka vyuo vikuu kuhakikisha vinazalisha wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu, pamoja na kuchimba na kuchakata rasilimali za nchi bila kutegemea kupita kiasi teknolojia kutoka nje.
Alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kukuza tafiti na ubunifu kupitia mipango mbalimbali, ikiwemo Mfuko wa Ubunifu wa Samia (Samia Innovation Fund), uanzishwaji wa shule za sayansi kwa wasichana na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi.
Maadhimisho ya miaka 40 ya COSTECH, yaliyozinduliwa Julai 2 mwaka huu, yanatarajiwa kuhitimishwa Novemba 17 na 18 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga maadhimisho hayo.
Shughuli zitakazofanyika ni pamoja na maonesho ya bunifu mbalimbali za kisayansi zilizozalishwa nchini pamoja na mbio za hisani zinazolenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika masuala ya sayansi na teknolojia.



