Serikali yatoa maelekezo udhibiti Ebola

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa maelekezo manne kwa wataalamu wa afya na viongozi wa serikali wa Mkoa wa Kagera.

Ummy alitoa maelekezo hayo jana jioni baada ya kukagua mpaka wa Murongo wilayani Kyerwa, ambapo jumla ya watu 11,500 wamepimwa viashiria vya ugonjwa wa Ebola katika mpaka huo.

Akitoa maelekezo hayo, Waziri Ummy ameiagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya zote za Kagera kuimarisha doria kwenye mipaka zaidi ya 1000 isiyo rasmi.

” Hapa Kagera kuna mipaka isiyo rasmi zaidi ya 1,000, hapa Kyerwa peke yake  kuna mipaka isiyo rasmi 32, tusijidanganye tunadhibiti hapa Murongo, mipaka mingine ambayo ni rasmi wakati njia za panya kibao watu wanapita tena ni wengi, lazima  mianya yote  idhibitiwe,” amesema Ummy.

Pia ameagiza  elimu zaidi itolewe kwa umma  hasa kwa waganga wa kienyeji na waendesha bodaboda.

“Kipindi cha Corona tuliona watu wengi wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji, jamani Ebola ni mbaya, Corona wote tumeumwa lakini tuligangamala, lakini Ebola ni hatari zaidi ndugu zangu na inaua haraka, waganga waelimishwe mgonjwa anapoenda basi atoe taarifa au kumshauri kwenda kituo cha afya,” amesema.

Pia amepiga marufuku wananchi hususani wafanyabiashara  kutokwenda wilaya ya jirani ya Mubende, iliyoripotiwa kuwa na mlipuko  mkubwa wa wagonjwa wa Ebola nchini Uganda kama hakuna shughuli ya dharura.

“Kama hakuna shughuli ya dharura msiende huko, ndugu zangu tujitahidi kuzuia maambukizi yasiingie nchini mwetu,  gharama za kuudhibiti ugonjwa ili usiingie ni kubwa, lakini ugonjwa ukishaingia gharama za kuudhibiti ni kubwa zaidi.

“Mtu akiupata ni rahisi kuusambaza kwa watu wengine na kati ya watu 10 wenye ugonjwa, wanne wanafariki, je mngependa kuona miongoni mwenu mnampoteza mwenzenu?

” Alihoji.

Waziri Ummy ameagiza kujengewa jengo maalum la kusubiria wahisiwa ambalo litakua lina huduma zote ikiwemo vyoo na maji.

“Hapa Murongo  kuna mahema ni sawa lakini wakati muhisiwa mnamsubirisha akitaka kwenda chooni anatumia choo gani?” Alihoji Ummy na kuongeza:

“Anaenda kule sokoni na atachangia na watu wengine, naiona hatari kubwa, ni lazima hatua za haraka zichukuliwe lijengwe jengo la dharura lenye huduma zote.”

Awali, akitoa taarifa ya mwenendo wa viashiria vya ugonjwa wa Ebola katika mpaka wa Murongo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Wilaya ya Kyerwa, Lewanga Msafiri, amesema kuanzia Septemba 20 hadi Oktoba 5, 2022 watembea kwa miguu waliopimwa ni 600 wakati wenye magari ni 500.

“Hata hivyo wote tuliowapima hawana viashiria na wale tuliowahisi wana joto lisilo la kawaida hatujawaruhusu kuingia nchini,” amesema Msafiri

Mpaka wa Murongo kuna soko kubwa la kimataifa la ndizi, ambalo linawakutanisha wafanyabiashara wa nchi za Tanzania, Uganda, Sudan, Rwanda na Burundi.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Ummy amewatoa hofu wafanyabiashara hao pamoja na Watanzania kuwa ugonjwa bado haujaingia nchini, lakini tahadhari kubwa zichukuliwe ikiwemo kunawa mikono na sabuni na maji tiririka.

Habari Zifananazo

Back to top button