Serikali yavuna bil 3/- madini miezi 8 Kagera

MAKUSANYO ya maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini katika Mkoa wa Kagera yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai 2024/ 2025 ni Sh Bilioni 3.2.
Kagera ilipangiwa kukusanya Sh bilioni 5.8 na mpaka mwishoni mwa mwezi Februari, 2025 imekusanya kiasi hicho cha fedha kikiwa ni sawa na asilimia 82 ya lengo.
Akizungumza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kagera, Nobert Mkopi amesema fedha hizo zimekusanywa kutokana na jitihada mbalimbali walizofanya katika usimamizi wa Sekta ya Madini katika halmashauri zote saba za mkoa huo.
“Mkoa wa Kagera kwa maana Sekta ya Madini tunasimamia halmashauri zote saba kwa maana ya wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba, Biharamulo na Ngara, kuna shughuli mbalimbali za uchimbaji madini. Mkoa huu yanapatikana madini mbalimbali ikiwemo bati, dhahabu, nickel, wolframite (WO3), madini ya viwandani na madini ujenzi,” amesema Mkopi.
Amesema maeneo ya Kyerwa yanachimbwa madini ya bati kihalali kwa leseni za uchimbaji mdogo lakini pia kuna leseni kubwa ya utafiti na madini yanayochangia asilimia 32 mpaka sasa ya maduhuli yaliyokusanywa ya Sh bilioni 3.2 na fedha nyingine zinatoka kwenye madini mengine ikiwemo dhahabu na ada mbalimbali za vibali na leseni.
Aidha Mkopi amesema mwenendo wa ukusanyaji maduhuli sio mbaya na hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wana imani watafikia lengo lililokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Mkopi ametoa wito kwa wawekezaji kote nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini mkoani Kagera ambako kuna utajiri mkubwa wa madini mbalimbali ikiwemo bati, dhahabu, nickel, wolframite (WO3), madini ya viwandani na ujenzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button