Serikali kuwekeza bilioni 350 kukabili tabianchi

SERIKALI ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 350 katika kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuongeza uzalishaji na kuimarisha uchumi wa taifa. Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kilimo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, alisema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza tija na kumuinua mkulima mdogo.
Amesema kwa sasa kuna zaidi ya miradi 750 ya kilimo inayoendelea nchini, huku Serikali ikilenga kufikia hekta zaidi ya milioni tano za ardhi ya umwagiliaji ifikapo mwaka 2030. Mweli ameongeza kuwa Serikali imeanzisha zaidi ya vituo 1,000 vya zana za kilimo nchi nzima ili kuwawezesha wakulima kupata zana za kisasa kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Afisa wa FAO Kanda ya Afrika, Mack Fynn, alisema mkutano huo unalenga kuboresha upatikanaji wa zana za kilimo kwa wakulima wadogo ili kukabiliana na changamoto za uzalishaji ikiwemo mabadiliko ya tabianchi. SOMA: Mashirika ya vijana yafundwa kukabili mabadiliko tabianchi
Naye mkulima kutoka Kilosa, Frola Elias, alisema matumizi ya zana za kisasa yatapunguza kazi ngumu na kuongeza ufanisi, huku akiomba vijana watengewe maeneo maalum ya kilimo ili kuongeza ushiriki wao katika sekta hiyo.



