SERIKALI imetenga Sh bilioni 4 katika bajeti ya maendeleo mwaka 2022/23 kwa ajili ya kukamilisha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji wa ekari 2,500 kikosi ya Chita JKT.
Haya yamebainishwa bungeni leo na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Khamis Hamza Chillo, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Felista Njau(CCM) aliyejibu kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax.
Katika swali lake, Njau alitaka kujua Mpango wa Serikali wa kuwawezesha kifedha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ili iweze kutekeleza kwa ufanisi mradi mkubwa wa kilimo cha mpunga Chita JKT – Morogoro na Shamba la Mngeta.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis, amesema Serikali inaendelea kuliwezesha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kifedha kila mwaka, ili liweze kutekeleza kwa ufanisi shughuli zake, ikiwa ni pamoja na miradi ya kilimo cha umwagiliaji katika shamba la mpunga lililopo Chita mkoani Morogoro na Shamba la Mngeta.
Amesema katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, serikali ilitoa Sh bilioni 4, ambazo zimetumika kununulia zana na vifaa vya kilimo kwa ajili ya shamba la Chita.
Amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023, serikali imetenga Sh bilioni 4 katika bajeti ya maendeleo, kwa ajili ya kumalizia awamu ya kwanza ya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji wa ekari 2500 huko Chita.
Amesema katika kuliendeleza shamba la Mngeta, lenye ekari 12,000, kiasi cha Sh 11,556,734,500, kinahitajika kwa ajili ya ununuzi wa zana, matengenezo na maboresho ya miundombinu ya uzalishaji, na gharama za uendeshaji.
Amesema Wizara inaendelea kufanya mazungumzo na Wizara ya kilimo, ili kuona uwezaekano wa shamba la Mngeta, kuwa sehemu ya mpango wa skimu za umwagiliaji, na taratibu za ndani zinaendelea ili kuwasilisha maombi ya fedha Wizara ya Fedha na Mipango.